Kilwa. Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema Bandari ya Uvuvi inayojengwa wilayani Kilwa Mkoa wa Lindi ni mradi wa kimkakati utakaoleta ajira kwa vijana sambamba na kuongeza pato kwa Taifa.
Ulega mesema tayari ujenzi wake mpaka sasa umefikia asilimia 63.
Akizungumza leo Jumanne Julai 30, 2024, alipotembelea mradi huo, Waziri Ulega amesema mpaka kukamilika kwake, ujenzi huo utagharimu Sh289 bilioni zikiwa ni fedha za ndani za Serikali.
“Nimeridhishwa na ujenzi unavyoendelea, hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 63, na mkandarasi amelipwa asilimia 40. Niwaombe vijana msifanye kazi kwa mazoea, huu mradi tunataka hadi ifikapo Februari 2025 uwe umekamilika na watu wapate ajira,” amesema Ulega.
Amesema mradi huo unapaswa kutazamwa kama mboni kwa kila mpenda maendeleo na ukikamilika utunzwe kusudi uwe endelevu.
Waziri huyo amesema kukamilika kwake utasaidia kuinua uchumi wa Mkoa wa Lindi sambamba na Taifa kwa jumla.
Awali, akizungumzia mradi huo, msimamizi wake kutoka Wizara ya Uvuvi, George Kwandu alisema maelekezo waliyopewa na Waziri Ulega wameyapokea na watayafanyia kazi kwa lengo la kufikia malengo ya Serikali.
“Ametuelekeza mambo mbalimbali ya kufanya ikiwamo ubora wa kazi, kumaliza mradi kwa wakati, watumishi wanaofanya kazi kwenye mradi huu wasiwe na malalamiko,” amesema Kwandu.
Moza Salumu, mkazi wa Kilwa Masoko ameishukuru Serikali kwa jitihada za ujenzi wa mradi huo kwa kuwa unakwenda kuwapatia ajira za muda na za kudumu.
“Huu mradi utatusaidia sana hasa sisi vijana na mama zetu, tutapata fursa ya kufanya biashara za aina mbalimbali kwa sababu watu watakuja wengi kutoka sehemu mbalimbali,” amesema Salumu.
Mpaka sasa, vijana 570 wamepata ajira kwenye ujenzi wa mradi huo wa bandari ya uvuvi na imeelezwa utakapokamilikia, vijana 30,000 watapata ajira kutoka sehemu mbalimbali hapa nchini Tanzania.
Sekta ya uvuvi nchini inachangia asilimia 1.8 kwenye pato la Taifa na malengo ya Serikali yanataka ifikapo mwaka 2036/2037 ichangie kwa asilimia 10.