Na Chedaiwe Msuya,WF-Mtwara
Wafanyabiashara wametakiwa kujenga tabia ya kuweka akiba katika biashara zao ili kuhakikisha wanakuwa na maendeleo endelevu.
Afisa Sheria Mwandamizi kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Ramadhani Myonza, alitoa wito huo alipokuwa akitoa elimu ya utunzaji na matumizi sahihi ya fedha katika ziara ya utoaji elimu ya fedha kwa umma wilayani Masasi mkoani Mtwara.
Akitoa elimu hiyo ya fedha, Myonza aliwasisitiza wafanyabiashara kujiepusha na matumizi ya pesa zote wanazozipata na badala yake waweke akiba ya sehemu ya mapato yao.
“Ndugu wafanyabiashara, tujenge tabia ya kujiwekea akiba katika biashara au katika mapato tunayopata katika utafutaji wetu,” alisema Myoka.
Alitoa mfano wa mfanyabiashara anayepata Sh 100,000, anashauriwa kutumia shilingi elfu sitini na kuweka Sh 40,000 kama akiba kwani itamsaidia baadaye.
Aliwaasa wafanyabiashara kuacha tabia ya kutumia pesa zote kwa kisingizio cha kujipongeza, kwani kufanya hivyo kunawarudisha nyuma kimaendeleo.
Kaimu Afisa Maendeleo ya Jamii, Ambros Ngwadakulima, eneo la Kilimanihewa amewaeleza wananchi wa Mkoa wa Mtwara kutoa ushirikiano kwa wataalamu na kuwaasa kujiunga katika vikundi vilivyokuwa rasmi, pia alisistiza wale wote wanaotoa huduma za fedha kinyume na utaratibu wa kisheria kuchukuliwa hatua.
Maisha Raimondi, mfanyabiashara kutoka kijiji cha Makanga, alitoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwaruhusu wataalam kutoka Wizara ya Fedha kuzunguka mikoani kutoa elimu ya utunzaji na matumizi sahihi ya pesa.
Alisema kuwa elimu hiyo itawasaidia sana wafanyabiashara kuendesha biashara zao kwa mafanikio na kuhakikisha kunakuwa na maendeleo endelevu.
Katibu wa vikao, Ismail Rashidi, kutoka Kata ya Kilimanihewa, ameipongeza Serikali kwa kutambua kuwa mkoa wa Mtwara kuwa miongoni mwa wanufaika wa elimu hiyo.
Aliendelea kusisitiza umuhimu wa wananchi wa Kilimanihewa kuacha tabia ya matumizi mabaya ya fedha na kuwekeza katika taasisi zilizosajiliwa ili kuhakikisha usalama wa fedha zao.
Afisa Mkuu wa Bima kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Gladness Lema, aliwahimiza wananchi kuwa na bima itakayoweza kuwasaidia katika maafa mbalimbali yatakayojitokeza katika shughuli za kilimo na kuweza kupata fidia kutokana na bima watakayoikata.
Wataalam hao walisema kuwa Mtwara ni mkoa wa tisa tangu wameanza kutoa elimu hiyo, wakitimiza maagizo ya Rais kupitia Wizara ya Fedha kuzunguka nchi nzima kutoa elimu ya fedha.