Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika maeneo mengi nchini zinatarajiwa kukoma Aprili 28, 2024.
TMA imesema mifumo inayosababisha viashiria vya mvua kubwa inaenda kudhoofu.
Meneja wa Utabiri wa TMA, Dk Mafuru Kantamla amesema hadi kufikia Aprili 28, 2024 mifumo inaonyesha hali ya mvua kubwa itakoma.
Hiyo ni habari njema kwa wananchi wa maeneo mengi nchini waliokumbwa na mafuriko.
Akizungumza na Mwananchi leo Aprili 25, 2024 Kantamla amesema, kuanzia Jumapili hali itakuwa shwari na katika maeneo mengi mvua kubwa itakoma.
Amesema wiki ya pili ya Mei, 2024 kutakuwa na upungufu mkubwa wa mvua kwenye maeneo mengi nchini, huku yale yanayopata mvua za masika ambazo ni za msimu zitaelekea kumalizika.
Kantamla amewataka wananchi hususani wanaoishi mabondeni kuchukua tahadhari kwa siku ambazo bado kuna mvua kubwa.
“Wananchi waendelee kufuatilia taarifa za TMA na kuchukua tahadhari stahiki, hasa wale ambao wako kwenye maeneo ya bondeni, ikiwezekana wachukue hatua ya kuondoka maeneo hayo,” amesema.
Amesema wananchi wanapaswa kutekeleza maelekezo ya taasisi zinazojihusisha na masuala ya maafa.
Kwa mujibu wa taarifa ya TMA iliyotolewa leo Aprili 25, kwa siku ya kesho Aprili 26, 2024 angalizo la mvua kubwa limetolewa kwa maeneo machache ya mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia) Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Kagera, Geita, Mwanza, Mara, Shinyanga, Simiyu, Kigoma, Tabora, Katavi na Rukwa pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.
TMA pia imetoa angalizo la upepo mkali unaofikia kilomita 40 kwa saa na mawimbi makubwa yanayofikia mita mbili kwa baadhi ya maeneo ya ukanda wote wa pwani ya Bahari ya Hindi (mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Lindi na Mtwara pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.
Kwa Jumamosi Aprili 27, 2024 angalizo la mvua kubwa limetolewa kwa maeneo machache ya mikoa ya Tanga, Kigoma, Tabora na Katavi pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.
Pia kumetolewa angalizo la upepo mkali unaofikia kilomita 40 kwa saa na mawimbi makubwa yanayofikia mita mbili, kwa baadhi ya maeneo ya ukanda wote wa pwani ya Bahari ya Hindi (mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Lindi na Mtwara pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.
Kwa Jumapili Aprili 28 na Jumatatu Aprili 29, 2024 TMA imetoa angalizo la upepo mkali unaofikia kilomita 40 kwa saa na mawimbi makubwa yanayofikia mita mbili, kwa baadhi ya maeneo ya ukanda wote wa pwani ya Bahari ya Hindi (mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Lindi na Mtwara pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.
Mvua kubwa za EL-Nino zilizoambatana na upepo mkali, mafuriko na maporomoko ya udongo katika maeneo mbalimbali nchini zimesababisha vifo vya watu 155 na wengine 236 kujeruhiwa.
Katika taarifa ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa hapo kuhusu changamoto za hali ya hewa nchini bungeni leo Aprili 25, 2024 mbali ya hayo, mvua zimesababisha uharibifu wa mazao, makazi, mali za wananchi, miundombinu kama vile barabara, madaraja na reli.
“Kutokana na athari hizo, zaidi ya kaya 51,000 na watu 200,000 waliathirika,” amesema.
Majaliwa amesema nyumba zaidi ya 10,000 ziliathirika kwa viwango tofauti.
“Maeneo mengine yaliyoathirika ni miundombinu ya shule, zahanati, nyumba za ibada, barabara, madaraja, mifugo na mashamba yenye mazao mbalimbali,” amesema.