RCO Tanga ashikilia dhamana ya kada wa Chadema

Dar es Salaam. Dhamana ya kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mkoani Tanga, Kombo Mbwana imezuiwa.

Kombo aliyepotea kwa takribani mwezi mzima kabla ya Jeshi la Polisi kutangaza ndilo linalomshikilia, alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Tanga, Julai 16, 2024, saa 11.00 jioni na kusomewa mashtaka chini ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta.

Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo Moses Maroa, alisema dhamana iko wazi kwa masharti ya kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Sh2 milioni kila mmoja, wenye barua ya mtendaji wa mtaa wanakoishi na vitambulisho vya Taifa.

Hata hivyo, alipelekwa mahabusu kwa kushindwa kutimiza masharti ya dhamana baada ya kukosa wadhamini kwa kuwa ndugu zake hawakuwa na taarifa wakati anapandishwa kizimbani.

Leo Jumanne, Julai 30, 2024 kesi iliitwa mahakamani na ndugu zake walikuwapo ili kumwekea dhamana wakiwa na nyaraka zilizohitajika.

Hata hivyo, mahakama imeshindwa kumpa dhamana baada ya Polisi mkoani Tanga kuomba asipewe dhamana.

Kesi hiyo iliitwa chemba ambako waliingia mawakili pekee ikielezwa hakuna nafasi ya watu wengine kuingia.

Ndugu wa mshtakiwa wakiwamo wazazi wake na mkewe pia hawakuingia.

Baada ya kesi kumalizika, mawakili watatu wa Kombo akiwamo Deogratius Mahinyila, walizungumza na ndugu wa mshtakiwa na waandishi wa habari wakieleza upande wa mashtaka umewasilisha kiapo cha Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Tanga (RCO), akiomba mshtakiwa asipewe dhamana. Mawakili wengine wa utetezi waliokuwapo ni Michael Rugina na Rachael Sadiki.

“Wakili wa Serikali, Paul Kusekwa amesema kuwa upelelezi wa shauri hili haujakamilika,” amedai.

Wakili Mahinyila amedai RCO wa Tanga amewasilisha kiapo akiomba mshtakiwa  asipewe dhamana, kwa kuwa upelelezi unaendelea na wana lengo la kuongeza washtakiwa wengine walio maeneo mbalimbali.

Wakili Kusekwa hakuwa tayari kuzungumza lolote akisema kama upande wa utetezi wameeleza kilichojiri,  basi inatosha na kwamba yeye hawezi kuzungumza lolote kwa kuwa huo ni mwenendo wa Mahakama ambao bado haujakamilika mpaka uamuzi utakapotoka.

Wakili Mahinyila amedai wamepinga ombi hilo na kwamba mahakama imewataka wawasilishe kiapo kinzani kabla ya Agosti 12, 2024 na kwamba mahakama itasikiliza siku hiyo.

Katika kesi hiyo ya jinai namba 19759 ya mwaka 2024, Kombo anakabiliwa na shtaka la kushindwa kutoa taarifa za kutosha za akaunti ya kadi yake ya simu, kinyume cha kifungu cha 126 cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta.

Anadaiwa Julai 9, 2024 alikutwa akimiliki laini (kadi ya simu) ya Tigo yenye namba (ICCID) 8925502042093621824, iliyosajiliwa kwa jina la Shukuru Kahawa na kushindwa kutoa maelezo ya kutosha kuhusu umiliki wa laini hiyo.

Pia anadaiwa kushindwa kusajili laini ya simu ambayo awali ilikuwa inamilikiwa na mtu mwingine, na kushindwa kuripoti kuhusu mabadiliko ya laini ya simu.

Kombo alipandishwa kizimbani mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Julai 16, 2024, na kusomewa mashtaka hayo, ambayo aliyakana.

Kabla ya kupandishwa kizimbami siku hiyo, Kombo alitoweka tangu Juni 15, 2024, baada ya kuchukuliwa na watu wasiojulikana nyumbani kwake Kijiji cha Kwamsala, wilayani Handeni, mkoani Tanga.

Julai 14, 2024 Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Zakaria Bernard alitangaza kuwa wanamshikilia.

Related Posts