NDANI ya Yanga kuna kazi kwelikweli. Unaweza kusema Kocha Mkuu wa kikosi hicho, Miguel Gamondi ni kama yupo katika wakati mgumu akikuna kichwa namna ya kupanga kikosi chake cha kazi, lakini upande mwingine, mastaa wa timu hiyo wanabaki tumbo joto kupambania namba zao.
Hiyo inatokana na namna usajili wao ulivyofanyika kipindi hiki cha dirisha kubwa huku asilimia kubwa wakimaliza kila kitu kuunda kikosi chao na majibu tumeyaona kwenye pre-season kule Afrika Kusini.
Maingizo mapya ndani ya kikosi cha Yanga ni Khomeny Abubakari (kipa), Chedrack Boka (beki wa kushoto), Clatous Chama, Aziz Andabwile na Duke Abuya (wote viungo), wakati Prince Dube na Jean Baleke wakiwa washambuliaji.
Nyota hao wamekuja kuongeza ushindani wa namba ndani ya kikosi hicho jambo ambalo linamfanya kila mmoja kuhitaji kujituma zaidi ili kumshawishi Kocha Gamondi ampatie nafasi.
Gamondi amefichua jambo akisema hivi sasa Yanga ikicheza, benchi kuna watu wa maana sana hivyo inampa wakati mzuri wa kuwasilisha mbinu zake wakati wa kusaka ushindi.
“Kwa sasa Yanga ina benchi imara zaidi, kila mmoja anaweza kucheza inavyotakiwa. Nina wachezaji 27 katika timu, siwezi kuwatumia wote mara moja, wanapaswa kuanza 11 na hao inategemea na mpinzani wetu yupoje,” alisema Gamondi na kuongeza:
“Kitu kikubwa ninahitaji kuona timu ikicheza vizuri na kushinda, suala la nani acheze inategemea na amefanyaje mazoezini wakati wa maandalizi.”
Yanga ambayo alfajiri ya jana ilirejea Dar es Salaam ikitokea Afrika Kusini ikiwa na Kombe la Toyota, ilicheza mechi tatu nchini humo na kufanya balaa kubwa ikishinda mbili na kupoteza moja huku ikifunga mabao sita na kuruhusu mawili pekee ikiondoka na clean sheet mbili na kombe mkononi.
Ilianza kwa kufungwa mabao 2-1 dhidi ya wakali kutoka Ligi Kuu ya Ujerumani, Augsburg lakini kiwango walichokionyesha siku hiyo kiliwaachia maswali mengi Wazungu.
Kocha wa Augsburg, Jess Thorup alisema: “Yanga wana timu nzuri, kuna ubora wa mchezaji mmojammoja ambao wana vipaji, wapo haraka, wana spidi, walifunga bao zuri kwa kichwa dhidi yetu. Ni timu yenye uzoefu na tumefurahi kucheza nayo.”
Katika mchezo huo dhidi ya Augsburg wa Kombe la Mpumalanga, Gamondi alianza na kikosi kazi hiki hapa; Djigui Diarra, Yao Kouassi Attohoula, Nickson Kibabage, Dickson Job, Ibrahim Hamad ‘Bacca’, Mudathir Yahya, Maxi Nzengeli, Clatous Chama, Clement Mzize, Stephane Aziz Ki na Salum Abubakar ‘Sure Boy’.
Mabadiliko kadhaa yalifanyika ambapo Chadrack Boka, Duke Abuya, Bakari Mwamnyeto na Aziz Andabwile waliingia wakati kipindi cha pili kinaanza. Baadaye Prince Dube, Jean Baleke, Jonas Mkude na Shekhan Khamis nao wakapata nafasi.
Picha iliyoonekana katika mchezo huo wa kwanza ilionyesha wazi kwamba Yanga ina timu ya maana kutokana na wale walioanza na waliotokea benchi, wote walikuwa moto wa kuotea mbali kwani Jean Baleke ambaye ni usajili mpya ndiye aliyepachika bao hilo akiwa ametumia dakika takribani 22 pekee tangu aingie.
Mchezo wa pili dhidi ya Wasauzi, TS Galaxy, usajili mpya Prince Dube ukaleta shangwe Jangwani baada ya kufunga bao pekee naye akiwa ametokea benchi ambapo Yanga ilianza na kikosi kilichoonekana ni cha pili. Kikosi hicho ni Aboutwalib Mshery, Kibwana Shomari, Farid Mussa, Dickson Job, Aziz Andabwile, Jonas Mkude, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Mudathir Yahya, Clement Mzize, Shekhan Khamis na Denis Nkane.
Ukiangalia kikosi hicho, Job, Mzize, Sure Boy na Mudathir ndiyo waliokuwepo pia katika kile kilichoanza dhidi ya Augsburg, waliobaki walitokea benchi na wengine hawakucheza kabisa mechi ya kwanza.
Kutokana na utajiri alionao Gamondi, nje aliwaacha Khomeny Abubakar, Djigui Diarra, Bakari Mwamnyeto, Ibrahim Bacca, Yao Kouassi Attohoula, Nickson Kibabage, Khalid Aucho, Maxi Nzengeli, Duke Abuya, Clatous Chama, Aziz Ki, Jean Baleke na Prince Dube.
Funga kazi ilikuwa mechi ya mwisho ambayo iliwapa Kombe la Toyota waliposhinda 4-0 dhidi ya Kaizer Chiefs, inayonolewa na Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi aliyemuachia kijiti Gamondi ndani ya Yanga.
Djigui Diarra, Yao Kouassi Attohoula, Nickson Kibabage, Dickson Job, Ibrahim Bacca, Khalid Aucho, Duke Abuya, Maxi Nzengeli, Clement Mzize, Aziz Ki na Prince Dube ndiyo kikosi ambacho Gamondi alianza nacho na kuonekana ndiyo cha kazi kwelikweli kwani kipindi cha kwanza kilimalizika kwa kufunga mabao 2-0, hadi inafika dakika ya 63, ubao ulisoma 4-0 matokeo ambayo yalibaki mpaka mwisho.
Kati ya wachezaji 27 waliopo Yanga kwa ajili ya msimu wa 2024-2025, Pacome Zouzoua, Kennedy Musonda na Khomeny Abubakar pekee ndiyo hawakupata nafasi ya kucheza hizo mechi za kirafiki. Khomeny alikuwa benchi katika mechi zote, wakati Pacome akichelewa kujiunga na kambi baada ya kwenda kwao Ivory Coast kushughulikia pasi yake ya kusafiri, huku Musonda ikielezwa alikuwa na matatizo ya kifamilia.
Katika kila nafasi ndani ya Yanga, kuna wachezaji zaidi ya wawili wanaoweza kucheza hapo. Golini makipa wote watatu wana ubora mkubwa ingawa wanapishana kidogo viwango wenyewe kwa wenyewe lakini yeyote atakayeaminiwa analiamsha vizuri.
Ukija katika beki wa kulia, Kibwana na Yao ndiyo nafasi yao halisi, lakini Gamondi pia anaweza kumtumia Job kucheza eneo hilo, wakati mwingine hata Maxi Nzengeli anayechezeshwa kama ‘wing back’ akizuia na kushambulia kutokea pembeni.
Upande wa beki ya kushoto, Boka na Kibabage ndiyo eneo lao, lakini Farid Mussa anaweza kutumika hapo, pia wakati mwingine hata Maxi, wawili hao wana uwezo wa kucheza kama ‘wing back’.
Eneo la ulinzi wa kati, Dickson Job, Bakari Mwamnyeto na Ibrahim Bacca wanachuana hapo, wameongezewa Aziz Andabwile ambaye kiuhalisia ni kiungo mkabaji akiwa na uwezo wa kucheza beki wa kati kama ilivyokuwa dhidi ya TS Galaxy na kulinda clean sheet.
Balaa lipo katika viungo ambapo kuna mchanganyiko wa viungo wakabaji na viungo washambuliaji ambao humo ndani wapo mawinga pia.
Aziz Andabwile, Salum Abubakar, Jonas Mkude, Mudathir Yahya, Khalid Aucho wana asili ya kiungo cha ukabaji, wakati Denis Nkane, Farid Mussa na Maxi Nzengeli ni mawinga huku viungo washambuliaji ni Shekhan Khamis, Clatous Chama, Pacome Zouzoua, Duke Abuya, na Stephane Aziz Ki.
Washambuliaji wapo Kennedy Musonda, Jean Baleke, Prince Dube na Clement Mzize. Tumeona tayari Dube na Mzize ni kama wana namba tayari kutokana na mechi tatu za pre-season walizocheza, kazi kubwa ipo kwa Musonda ambaye anahitaji kufanya juhudi kubwa ili acheze.
Mzize na Baleke kila mmoja amefunga bao moja kati ya sita yaliyofungwa na Yanga pre-season wakati Dube anayo mawili katika mechi tatu walizocheza wakiwa Afrika Kusini. Mwingine aliyefunga ni Aziz Ki mawili.
MAKIPA: Djigui Diarra, Aboutwalib Mshery, Khomeny Abubakar
MABEKI: Kibwana Shomari, Yao Kouassi Attohoula, Chadrack Boka, Nickson Kibabage, Dickson Job, Bakari Mwamnyeto na Ibrahim Bacca.
VIUNGO: Aziz Andabwile, Denis Nkane, Farid Mussa, Salum Abubakar, Jonas Mkude, Shekhan Khamis, Mudathir Yahya, Clatous Chama, Pacome Zouzoua, Duke Abuya, Khalid Aucho, Maxi Nzengeli, Stephane Aziz Ki
WASHAMBULIAJI: Kennedy Musonda, Jean Baleke, Prince Dube, Clement Mzize