Dar es Salaam. Kutokana na hitilafu ya umeme iliyojitokeza kati ya Stesheni ya Kilosa na Kidete na kusababisha treni ya SGR iliyokuwa inasafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma kusimama kwa muda wa saa mbili huku ngedere, bundi wakitajwa.
Kwa mujibu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), hitialfu hiyo ilitokea jana Julai 30, 2024.
“Shirika la Reli Tanzania (TRC) linaomba radhi kufuatia hitilafu ya umeme iliyojitokeza kati ya Stesheni ya Kilosa na Kidete na kusababisha treni ya WI ya kiwango cha kimataifa (SGR) iliyokuwa inasafiri kutoka Dar es Salaam kuelekea Dodoma kusimama kwa muda wa saa mbili (2) siku ya tarehe 30 Julai 2024.” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa za awali zinaonesha kuwa hitilafu aina hiyo husababishwa na wanyama (ngedere) au ndege (bundi) wanapogusa nyaya za umeme zilizotandazwa juu ya reli (overhead catenary system).
Aidhaa, hitilafu ilisababisha umeme kukatika kituo cha kupoozea umeme namba 7 (Godegode) na mafundi wa TRC walifanikiwa kutatua changamoto hiyo na kurejesha umeme saa 6:30 usiku na treni kuendelea na safari kuelekea Dodoma ambapo iliwasili mkoani humo saa 7:57 usiku.
Endelea kufuatilia Mwananchi.