Karma ina nafasi kutenguliwa kwa Nape, January

Utenguzi uliofanywa na Rais Samia, kuwatumbuaji mawaziri wake wawili vijana, maarufu kama watoto pendwa, umepokelewa kwa hisia tofauti, wengine wanapongeza na wengine wanaona kama wameonewa.

Mimi ni muumini wa kitu kinachoitwa karma, ambayo ni kanuni ya kila binadamu kuhukumiwa kwa mawazo yake, maneno yake na matendo yake, wazungu wanasema, “what goes around, comes around”.

Hivyo, utenguzi na utumbuzi wa mawaziri hao ni matokeo ya mawazo yao, maneno yao na matendo yao, kutumbuliwa huko ni haki yao na stahiki yao.

Uteuzi unafanywa kwa ridhaa ya mteuzi na kutenguliwa pia ni ridhaa ya mteuzi, na sio kwa stahili na stahiki. Pia, kwenye kutenguliwa, unaweza ukatenguliwa bila kosa lolote na mteuzi akawa hajafanya kosa lolote kwa sababu uteuzi na utenguzi ni kwa ridhaa ya mamlaka ya uteuzi.

Lakini kwenye kutumbuliwa lazima mtu ufanye kosa la kustahili kutumbuliwa, ukitumbuliwa kwa uonevu, hiyo karma itaingilia kati kukufidia na kukulipia.

Mfano, kutumbuliwa kwa Nape, inawezekana kabisa ni mkusanyiko wa karma za mabao ya mkono yote aliyoyasimamia, hivyo ametumbuliwa kwa haki. Lakini kama ametumbuliwa kwa kosa la kuusema ule ukweli wa kinachofanyika kwenye uchaguzi, basi ameponzwa na mdomo wake, lakini kama alichokisema ni kitu cha kweli na huwa kinafanyika, basi ametumbuliwa kwa kuonewa, hivyo anatakiwa kufurahia na karma itamfidia na kumlipia.

Kwa vile Nape aliyatamka hayo kwenye jimbo la Stephen Byabato na Bukoba Mjini, je, Byabato kosa lake ni nini hadi kutumbuliwa? Inawezekana ni kauli ya Nape, hivyo Byabato ameponzwa na Nape bila yeye kufanya kosa lolote, hivyo ametumbuliwa kwa uonevu. Hivyo, Byabato anatakiwa kufurahi, atafidiwa na kulipiwa.

Kwa January, kiukweli sijui, kama ilivyokuwa kwa Balozi Liberata Mulamula, hadi leo sijawahi kujua sababu, lakini tayari yeye karma imemfidia, sasa ni mhadhiri mkazi wa diplomasia katika Chuo Kikuu cha John Hopkins kilichopo Marekani, ni jambo la fahari.

Kwa vile Rais Samia ameonyesha njia kwa kutuhisania, kututajia sababu za kuwateua baadhi wateule wake, tuwe watu wa shukrani kwanza kwa kumshukuru kwa hiyo hisani kwanza, kisha tumuombe siku anawatumbua, pia atupe haki ya kupata taarifa za sababu za kuwatumbua, asiishie kwenye kutupatia taarifa za uteuzi na utenguzi. Tupatiwe taarifa za sababu za utenguzi kwani viongozi hao ni watumishi wa umma wanaolipwa na fedha za umma, hivyo umma una haki zote za kujua kuhusu utendaji wa wateule hao na sababu za kutenguliwa au kutumbuliwa kwako.

Watanzania tufike mahali tupewe haki ya kupata taarifa wakati wa utenguzi au utumbuzi, kwa mfano, kama nilivyosema awali, hadi leo sijawahi kujua kwanini Balozi Mulamula alitumbuliwa, sasa January naye ametumbuliwa, natamani kujua sababu.

Kwa upande wa Nape, sihitaji kujua sababu ya kutumbuliwa kwake, ni dhahiri mdomo wake umemponza. Amesadifu ule usemi wa Kiswahili wa “mzaha mzaha, hutumbua usaha”. Hata hivyo, kwa Byabato, bado hatujui amekosa nini kustahili kutumbuliwa.

Nashauri tumsaidie Rais Samia aepuke kufanya uamuzi yatakayosababisha karma kufanya kazi yake bila kujijua, japo uteuzi na utenguzi ni kwa hisani tu, lakini ukimtumbua mtu bila haki, kwa namna inayomdhalilisha, huyo mtumbuliwa akiumia, anatengeneza karma ya maumivu yake, hiyo karma inahifadhiwa katika akiba ya karma ya aliyesababisha maumivu hayo. Hivyo, hii karma inaongezeka, ikifikia hatua ikajaa hadi furushi hilo likawa halibebeki, hilo zigo la karma litamuelemea mbebaji. Wakati mwingine linaweza kumponza, ndiyo maana nimewashauri viongozi wetu wateuliwa.

Wito kwa viongozi wetu, unapokosea, hata kwa kujikwaa tu ulimi, tujenge utamaduni wa kuwajibika ili kumuepushia Rais wetu kubeba mzigo wa karma.

Nape na January ni kama watoto tu kwa Rais Samia, mtoto akikosa, unamrudi, hivyo sasa amewarudi vijana hawa, tunamuomba wakijirudi, mwaka 2025 awasamehe, awaite tena kwa sababu kiukweli hivi vichwa ni hazina, ujana na mizaha mizaha ya utoto imewaponza, wakikua wakatulia, wana fursa kuja kuwa viongozi wakubwa wazuri.

Related Posts