Kauli za mwisho za mama mzazi wa Halima Mdee kabla ya mauti

Dodoma. Ndugu na watu wa karibu wa Theresia Mdee, mama mzazi wa Mbunge wa Viti Maalumu, Halima Mdee, wameelezea kauli za mwisho za marehemu kwao ni wapendane, wafanye kazi kwa bidii na wasimsahau Mungu katika maisha yao.

Theresia alifariki dunia asubuhi ya jana Jumanne Julai 30, 2024, katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, jijini Dodoma baada ya kuugua saratani ya shingo ya kizazi.

Jana usiku wa Jumanne, Mwananchi lilifika Area D jijini Dodoma ambako ndiko msiba ulipo na taratibu za mazishi zinafanyika na kukuta waombolezaji mbalimbali wakiwemo wabunge.

Joseph Mdee, kaka wa Halima amesema kinachowauma na kuwasikitisha ni jinsi mama yao dakika za mwisho duniani kuwaonea huruma kuwa anawaacha.

“Kitu ambacho kinaniuma na kunisikitisha alikuwa anaumia kuwaacha watoto wake. Alikuwa anapenda sana familia yake, alikuwa anaumia kutuacha. Ni mama bora sana, aliyekuwa anapenda wanae,” amesema.

Amesema familia ya Mdee haijapoteza mama tu bali ni rafiki katika maisha yao.

Joseph amesema kauli yake ya mwisho ya mama yake ni wapendane na waishi kwa amani kwa sababu familia nyingine huwa zinatofautiana baada ya kuondokewa na mmoja wa wazazi ama wazazi.

Amesema mama yao, ameacha watoto wanne, Halima akiwa mtoto wa pekee wa kike na wajukuu wanane.

Amesema mwili wa Theresia utasafirishwa kupelekwa jijini Dar es Salaam ambako ni nyumbani kwake, Agosti 1, 2024 na kisha kuelekea Wilaya ya Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro Agosti 5, 2024 kwa ajili ya mazishi.

Naye rafiki wa karibu wa Halima, Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Bulaya amesema Theresia alilazwa katika Hospitali ya Benjamin Mkapa Julai 8, 2024.

Hata hivyo, amesema juzi Jumatatu alizidiwa na kupelekwa Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU) na alifariki dunia saa 4 asubuhi ya jana Jumanne.

“Wiki iliyopita usiku alituambia wanangu mimi siponi…akatuambia pendaneni msigombane. Endeleeni kuishi kwa upendo lakini mcheni Mungu na kufanya kazi kwa bidii. Kikubwa nashukuru Mungu mmeniuguza Mungu awabari wanangu,” Bulaya amemnukuu Theresia. 

Amesema katika sekta ya siasa, Theresia wamepoteza mama ambaye alikuwa akiwasaidia kupambana katika changamoto zote walizopitia kwenye maisha ya kisiasa.

“Amekuwa akitutia moyo katika siasa. Ni mama ambaye anafuatilia, mimi nikiwa Bunda (Mara) ananiuliza unaendeleaje. Hata kabla ya kulazwa, mimi nilikuwa Bunda alinipigia simu na kuniuliza kama nimefika salama, akaniambia mwanangu mimi naumwa, nikamwambia narudi,” amesema.

Amesema hilo lilimfanya kusitisha ziara yake Bunda na kurudi Dodoma Julai 7, 2024 ambapo walimpeleka Hospitali ya Benjamin Mkapa Julai 8, 2024.

Bulaya amezikumbuka nyakati alizopata faraja kubwa kutoka kwa Theresia kuwa ni wakati walipokuwa mahakamani kwa ajili ya kesi za kufukuzwa uanachama wa Chadema ambapo alikuwa akihudhuria pamoja nao mahakamani.

Bulaya amesema anakumbuka alivyokuwa akiwarushia fedha katika simu kipindi ambacho walisimamishwa kuhudhuria vikao vya Bunge kwa mwaka mzima.

“Najua nyie hamna mishahara chukueni, sio kwamba hatuna bali ni mama ambaye anafahamu watoto wake hawako kazini kwa hiyo anakurushia fedha,” amesema.

Wabunge mbalimbali walifika kumfariji Mdee, wakiwemo wabunge wa viti maalum Salome Makamba, Jesca Kishoa na Kunti Majala na Sophia Mwakagenda.

Kwa upande wake, Mwakagenda amesema kwa wabunge 19 wa viti maalumu, Theresia alikuwa ni mama yao ambaye alikuwa akiwashauri wakati wanapokuwa na matatizo yao binafsi.

“Muda mwingi alikuwa anakuwa hapa Dodoma kwa hiyo tulikuwa tunafika kupata ushauri wa kimama. Na unafahamu kabisa yeye ni mtu mzima ambaye ameona maisha mengi. Sisi ni suala hili limetusikitisha sana,” amesema.

Related Posts