Kasi ya kufumania nyavu ambayo imeanza kuonyeshwa na wachezaji wapya waliosajiliwa na timu tofauti za Ligi Kuu Bara kwenye mechi za maandalizi ya msimu mpya (pre-season) hapana shaka inazipa imani chanya timu zao kwamba watakuwa na mchango mkubwa katika msimu ujao.
Tathmini iliyofanywa na gazeti hili kwa timu saba ambazo zimeshacheza mechi za kujipima nguvu na mashindano katika kipindi hiki cha maandalizi ya msimu mpya inaonyesha wachezaji wapya wametoa mchango mkubwa katika kupachika mabao kwa timu zao licha ya muda mfupi ambao wamezitumikia.
Hadi sasa, Yanga imecheza mechi tatu ambazo zote zilikuwa huko Afrika Kusini dhidi ya Augsburg ya Ujerumani na TS Galaxy ya Afrika Kusini katika Kombe la Mpumalanga, kisha ikacheza na Kaizer Chiefs katika Kombe la Toyota.
Katika mechi hizo tatu, Yanga imefunga idadi ya mabao sita ambapo kati ya hayo, matatu yamepachikwa na nyota wapya ambao ni Prince Dube aliyefunga mawili na Jean Baleke aliyefunga moja, mengine matatu yakifungwa na nyota waliokuwepo kikosini tangu msimu uliopita, Stephane Aziz Ki aliyefumania nyavu mara mbili na Clement Mzize mwenye moja.
Katika mechi hizo tatu, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Kaizer Chiefs, ikapata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya TS Galaxy na ikapoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Augsburg.
Azam FC imeshacheza mechi nne katika kipindi hiki cha maandalizi ambazo zote zilikuwa za kirafiki dhidi ya Zimamoto ya Zanzibar na dhidi ya timu tatu za Morocco ambazo ni Mansour, Touarga na Wydad AC.
Idadi ya mabao nane ndio yamefungwa na Azam FC kwenye mechi hizo nne ambapo manne yamefungwa na wageni, Jhonier Blanco aliyepachika matatu na Nassor Saadun aliyefunga moja, mengine manne yamefungwa na wenyeji ambao ni Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliyefunga mawili na Djibril Sylla na Cheick Sidibe waliofunga bao moja moja.
Azam iliichapa Zimamoto mabao 4-0, ikaifunga Mansour kwa mabao 3-0, ikalazimishwa sare ya bao 1-1 na Touarga kisha ikapoteza kwa mabao 4-0 dhidi ya Wydad AC.
Simba imecheza mechi tatu tangu ilipoanza maandalizi ya msimu mpya dhidi ya timu za Canal Suez, Telecom na Al Adalah ikiwa huko Misri.
Katika mechi hizo tatu, Simba imefumania nyavu mara saba, ambapo mabao sita yamefungwa na nyota wake wapya nao ni Charles Ahoua aliyefumania nyavu mara mbili huku Joshua Mutale, Augustine Okejepha, Valentino Mashaka na Steven Mukwala kila mmoja akifunga bao moja.
Mechi zote tatu, Simba ilipata ushindi ambapo iliifunga Suez Canal mabao 3-0, ikaiadhibu mabao 2-1 Telecom kisha ikapata ushindi kama huo dhidi ya Al Adalah.
Dodoma Jiji FC imecheza mechi tatu za kirafiki ikiibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mbuni, ikashinda 2-1 dhidi ya Singida Big Stars na kuichapa Namungo FC mabao 3-0, kati ya mabao hayo sita iliyopata, mawili yamefungwa na wapya Ibrahim Ajibu na Reliants Lusajo na mengine manne yakipachikwa na waliokuwepo tangu msimu uliopita, Mwana Kibuta, Iddi Kipagwile na Mwana Kibuta.
Singida Black Stars kipindi hiki imefunga mabao nane ambapo kati ya hayo, manne yamefungwa na wapya na manne yamepachikwa na wa zamani wakati KMC wamecheza mechi moja na kufunga mabao matano, matatu kati ya hayo yakifungwa na wapya na mengine mawili ya ambao walikuwepo kikosini msimu uliopita.
Coastal Union imecheza mechi tatu ikifunga mabao mawili ambayo moja limewekwa kimiani na mchezaji mpya na lingine la mchezaji wa zamani.
Kocha wa Simba, Fadlu Davids alisema kuwa anafurahishwa na maendeleo ya nyota wake wapya na hata wale wa zamani ingawa alisema wanahitajika kufanyia kazi zaidi uwezo wao kwa kutumia nafasi za mabao wanazotengeneza.
“Timu imeimarika kila eneo na wachezaji tayari wameanza kuingia kwenye mfumo shida ya kutofunga ni sehemu ndogo ambayo inaweza kuisha kwa muda mfupi kwani wachezaji wamekuwa wakijitenga vizuri kwenye nafasi,” alisema.
Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi alisema kufanya vizuri kwa nyota wapya kunaongeza wigo wa uteuzi wa kikosi chake cha mechi.
“Kwa sasa Yanga ina benchi imara zaidi, kila mmoja anaweza kucheza inavyotakiwa. Nina wachezaji 27 katika timu, siwezi kuwatumia wote mara moja, wanapaswa kuanza 11 na hao inategemea na mpinzani wetu yupoje,” alisema Gamondi.