KOCHA Mkuu wa Coastal Union, David Ouma amesema asilimia 70 kikosi chake kipo tayari kwa ajili ya kuanza msimu mpya huku akidai kuwa 30 zilizobaki ni za mbinu.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ouma ambaye yupo Pemba sambamba na timu hiyo, alisema maandalizi yanakwenda vizuri na wachezaji kwa asilimia kubwa wameingia kwenye mfumo.
“Kikosi kinaendelea vizuri na tayari tumepata nafasi ya kucheza mechi mbili za kirafiki zote tumeshinda. Ni mwendelezo mzuri wa pale tulipoishia msimu ulioisha,” alisema.
“Tumecheza na Chipukizi FC tumeshinda mabao 4-0, dhidi ya Tekeleza FC tumeshinda bao 1-0. Nafurahishwa na ubora wa wachezaji wangu waliofanya kazi kubwa msimu ulioisha na maingizo mapya ambayo taratibu yanazoeana na wenzao.”
Ouma alisema asilimia 70 za ubora aliouona anaamini timu hiyo ikirudi na ubora uleule waliouonyesha msimu ulioisha huku akiweka wazi kuwa hizo ni kwa uwezo wa wachezaji.
Alisema baada ya kuimarisha pumzi na wachezaji kujenga utimamu wa miili hivi sasa anapambana kumalizia asilimia 30 kwa ajili ya kuwaingiza kwenye mifumo.
“Kuna maingizo mapya licha ya kuweza kuanza vyema kwa kuonyesha uwezo mechi hizo tulizocheza, nina muda mfupi wa kukamilisha hizo asilimia 30 kwa kuhakikisha wachezaji wangu wote wanaingia kwenye mifumo yangu,” alisema.
Coastal Union msimu uliopita ilimaliza nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara na kupata nafasi ya kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ikiungana na Simba ambayo ilimaliza nafasi ya tatu.
Mabingwa wa ligi hiyo, Yanga na Azam FC iliyoshika nafasi ya pili zitaiwakilisha Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Afrika.