Dar es Salaam. Waliokuwa wapangaji katika nyumba zinazoathiriwa na mradi wa uendelezaji Bonde la Mto Msimbazi wenye mikataba na wasio nayo, wote watafidiwa Sh170,000.
Awali, Serikali ilisema ambao wangelipwa ni wale tu waliokuwa na mikataba, jambo lililozua malalamiko miongoni mwa wapangaji wakisema maisha ya maeneo hayo ingekuwa vigumu kuandikishiana mikataba.
Katika utekelezaji wa mradi huo unaogharimu Dola za Marekani milioni 260 (Sh675 bilioni), ukifadhiliwa na Benki ya Dunia (WB), wenye nyumba walifanyiwa tathmini na kulipwa, huku wapangaji wakiahidiwa malipo ya Sh170,000 kwa ajili ya kuwasaidia kusafirisha mizigo yao watakapokuwa wanahama.
Tayari Sh52.6 bilioni zimetengwa kwa ajili ya utoaji wa fidia na mpaka sasa watu 2,155 kati ya 2,329 wameshalipwa.
Akizungumza leo Alhamisi, Aprili 25, 2024, Ofisa Habari Mwandamizi wa Mradi wa Bonde la Msimbazi, Raphael Kalapilo amesema Serikali imeamua kubadili uamuzi na sasa itawalipa wapangaji wote waliokutwa ndani kipindi cha uthamini wa nyumba.
Moja ya vigezo watakavyoangalia ni ushahidi kutoka kwa majirani kama ni mtu waliyemfahamu kuishi kwenye nyumba husika.
“Tayari hatua hizo zimeanza za kuwaingiza kwenye malipo wapangaji 200 ambao walikuwa wameachwa, kazi iliyoanza leo kwa kutakiwa kujaza fomu maalumu kwa ajili ya malipo,” amesema Kalapilo
Akizungumzia hilo, mmoja wa wapangaji, Asia Fupe, amesema Serikali imefanya jambo la busara kwa kuwa walikuwa katika sintofahamu hasa pale walipochukuliwa taarifa zao, halafu baadaye yakaja majibu kwamba hawatalipwa.
“Tulikuwa tunajiuliza ilikuwaje mpaka wakatupiga picha na kuchukua taarifa zetu zingine huku wakijua hatutakuwa kwenye malipo, na kuhisi labda kuna upigaji unataka kufanywa, afadhali wametuondolea wasiwasi huo,” amesema Asia.
Khatibu Mohamed, mpangaji aliyekuwa akiishi Magomeni Suna, amesema bado hajapata taarifa ya kuitwa kusaini malipo, huku akieleza atafuatilia hilo.
Kalapilo amesema kwa ambaye hakupata ujumbe kutoka kwa mwenyekiti wake kuna mawili, ama alishajaza fomu hizo au si miongoni mwa wapangaji wanaopaswa kulipwa.
Amesema kuna wengine walipanga baada ya nyumba kuwa zimefanyiwa uthamini na kuwekwa alama.