Kocha Mkenya akabidhiwa MIKOBA Tabora United

TABORA United msimu ujao itakuwa chini ya Kocha Mkenya, Francis Kimanzi ambaye muda wowote atatambulishwa.

Kocha huyo wa zamani wa Tusker ya Kenya na timu ya Taifa hilo tayari amefikia makubaliano ya awali na Tabora United na kilichobaki ni kutua Tanzania kusaini mkataba wa mwaka mmoja waliokubaliana.

Kimanzi mwenye leseni ya UEFA daraja A anakuja kuinoa timu hiyo iliyonusurika kushuka daraja msimu uliopita akichukua mikoba ya Mrundi Masoud Juma ambaye aliondoka siku chache kabla ya mechi ya marudiano ya mchezo wa mchujo (play off).

Tayari kocha huyo ameutaka uongozi wa Tabora United kuipeleka timu jijini Dar es Salaam kuendelea na maandalizi ya msimu ujao na kwamba, ataanzia kazi huko huku maelekezo hayo yakifanyiwa kazi fasta kikiendelea kunolewa na kocha msaidizi.

“Tutakuwa na Kimanzi bodi ya klabu imeona ndiye kocha anayetufaa. Nadhani wiki hii ataanza kazi, amebakiza kuja tu nchini,” alisema mmoja wa mabosi wa Tabora United.

“Tulikuwa tunataka kocha mwenye uzoefu kidogo na soka la Afrika na Kimanzi ni mmoja wa makocha bora Afrika Mashariki.”

Related Posts