KATIKA mfululizo wa Mwanaspoti kukuletea simulizi tamu za mabondia wa ngumi za kulipwa, tumefunga safari hadi Bagamoyo mkoani Pwani kukutana na bondia Rehema Abdallah wa Sharifa Boxing Gym.
Siyo bondia mwenye jina katika mchezo wa ngumi lakini ndiyo bondia anayeshikilia rekodi ya kucheza mapambano mengi bila ya kupoteza kwa lugha ya majahazi tunasema ‘undefeated’
Imetuchukua saa moja na dakika 16 kwa umbali wa kilomita 66 kufika katika mji wa Kihistoria wa Bagamoyo kumpata bondia Rehema Abdallah.
Lakini siyo rahisi kwa wanamichezo wa kike nchini kumkuta amevalia mavazi ya kike na mara nyingi muda wote huwa wanapenda kuwa na kuonekana kiume kwa ma,ana ya mavazi ila kwa Rehema ilikuwa tofauti kutoka na kumkuta nyumbani alipopanga amevalia kijora tena akiwa jikoni.
Rehema anayeshikilia rekodi ya kucheza mapambano 11 akiwa ameshinda 10 kati ya hayo tisa ameshinda kwa ‘Knockout’ na ametoka sare katika pambano moja pekee na bondia Sijali John wakati huo alikuwa jikoni kupika wali kabla ya kubadilika kwenda mazoezini baada ya mazoezi ya asubuhi jambo ambalo siyo rahisi kwa wanamichezo wengi kukaa jikoni kuandaa vyakula vyao.
Mwanaspoti lilishangazwa na jambo hilo lakini kwa upande wa bondia huyo aliyepata ufadhili kwenda kuweka kambi fupi ya mazoezi nchini Urusi kwa ajili ya pambano lake dhidi ya Mwingereza mwenye asilia ya India, Sangeeta Birdi anasema kuwa moja ya jambo kubwa analopenda ni kupika kwani siyo rahisi kwake kula vyakula vya mama ntilie ikiwa mwenye ni mpishi mzuri.
Katika mahojiano ambayo yalianzia jikoni sehemu ambayo bondia huyo anaandaa chakula, Mwanaspoti lilitaka kujua jambo gani lilimfanya aingie kwenye mchezo wa ngumi za kulipwa.
“Kwanza mchezo wa ngumi kwangu nilianza mwaka 2017 hapa Bagamoyo ingawa haikuwa jambo rahisi kukubali kuingia huku.
“Kilichoniponza ni kwa sababu kuna sehemu nilikuwa naenda kupiga stori kwa sababu ya rafiki yangu anaitwa Body yeye ni muongozaji wa filamu za Kibongo sasa wasanii wakubwa alikuwa anawaleta kwa ajili ya kufanya nao kazi.
“Lakini wakati huohuo Body alikuwa na rafiki yake anaitwa Sharifa Muhsin ambaye ndiyo amekuwa meneja wangu akawa kila akienda kwa Body ananikuta ikabidi nimwambie Body kama anataka niingize kwenye mchezo wa ngumi.
“Body alivyoniambia nilikataa kwa sababu mwanzo kabisa nilijua ni mbinu za wanaume kwa sababu hisia zangu ziliniambia kwamba ni mtego wa kutaka kunitongoza, nikawa namkwepa kila ninapomuona Sharif.
“Lakini kuna siku alinikamata akaniambia kwa nini nimekuwa nikimkimbia. Sikuwa na cha kumjibu ila yeye akaniomba niende katika gym yake. Kweli nilienda siku ya pili na hapo ndiyo safari yangu ilianzia kwenye mchezo wa ngumi.
“Nilifanya mazoezi baada ya muda kupita nikacheza pambano langu la kwanza katika ngumi za kulipwa dhidi ya Enjoy Bryson. Nakumbuka ilikuwa Mei 20, 2017 nilimpiga kwa pointi japokuwa changamoto kwangu ilikuwa pumzi.
“Nikaendelea kucheza mapambano na Mungu akawa upande wangu ushindi ukawa napata wa KO hadi mwaka 2018 nilipotoroka na kuachana na ngumi bila kumwambia hata meneja wangu Sharifu.
Nini kilikufanya utoroke na kuacha ngumi?
“Unajua wakati ule nipigana pia nilikuwa najifunza mambo ya U-dj kwa sababu elimu yangu ni darasa la saba halafu nikaja kuona ngumi zinanichelewesha tofauti na wenzangu.
“Nilikuwa nacheza mapambano madogo lakini mabondia wengine wanasafiri kama Feriche Mashauri na Halima Vunjabei ila mimi nipo, pesa sipati, kiukweli ikanikatisha tamaa na kuamua kuacha ngumi.
“Wakati naacha lakini kulikuwa na mzee mmoja alikuwa anakuja kwenye sehemu ambayo najifunza U-DJ akanimbia ana ndugu zake nao ni madj wanafanya kazi katika moja ya baa za ndugu yake Boko niende nikaungane nao, nitakuwa DJ mzuri.
“Kweli niliondoka na hapo ndiyo ikawa mwanzo kuondoka Bagamoyo na kwenda kuanza maisha mapya Boko. Kazi yangu ikawa ni U-DJ kupiga muziki katika baa ya yule rafiki wa yule mzee alinileta Boko. Nadhani hakuna haja ya kuitaja jina.
Vipi U-DJ ulikuwa unalipa?
“Hapana kwa sababu hakuna kikubwa ambacho nilikuwa napata zaidi, maana madj tulikuwa watatu, hivyo tukawa tumegawana siku za kupiga na Dj mmoja kupiga mara tatu malipo ya siku ni Sh10,000.
“Lakini kuna wakati tunapiga wawili halafu tunagawanya Sh5,000 kwa kila mmoja ila siku za wikiendi ndiyo tulikuwa tunapata posho nyingi kwa sababu ya promo za kampuni ambayo pesa yote ukichanganya ndiyo unaweza kufikia Sh12,0000.
“Kiukweli mambo yalikuwa magumu ila kutokana ujanja wangu wa kujichanganya nikawa napiga kazi, ukonda wa daladala za Boko-Tegeta kwa siku ambazo nilikuwa siendi kupiga shoo ya UDJ na wakati mwingine nikawa naendesha bodaboda kwa kuwashikia watu ili nisiyumbe kiuchumi sasa.
“Unajua katika maisha binadamu tunakutana na watu wengi hapo nikapata mahusiano na dereva wa lori la mchanga halafu pia alikuwa dalali, mbaya zaidi alikuwa ni mume wa mtu.”
Hukujua kama ni mume wa mtu?
“Sikujua mapema ila nilikuja kujua baada ya kuwa mjamzito maana tulivyoingia kwenye mahusiano alinitoa kwenye kazi yangu ya udj kwa kuniahidi kunihudumia, akanipangia na chumba kabisa.
“Wakati wa ujauzito alitimiza majukumu yake kama baba ila baada ya mke wake kujua tena nilivyojifungua ndiyo mambo yakaharibika ikabidi nirudi Dodoma upande baba.
“Nilikaa Dodoma, lakini kuna ndugu yangu mmoja akanirudisha tena Dar nikiwa na mwanangu mdogo wa kike lakini niliona mambo magumu, ikabidi nimtafute rafiki wa meneja wangu anaitwa Nani Mfuko.
“Mfuko nilimueleza ilikuwa mwaka juzi akanimbia niende Bagamoyo ila hata nilivyofika nilienda moja kwa moja hadi Body nilimueleza changamoto yangu ila nilimwambia nataka kurudi Dodoma.
“Lakini alichofanya ni kunipeleka hadi kwa mjumbe kwa sababu hakuamini kama mtoto ni wangu. Tukaandika maelezo kwa lolote litakalotokea basi asitiwe hatiani, kisha akanitafutia hoteli ya kupumzika na mwanangu pamoja na mahitaji mengine kabla ya safari ya kurudi Dodoma.
“Sasa ilipofika jioni nikaenda kumuona Haji Mfuko yule rafiki wa meneja wangu Sharif ambaye nilikuwa namuogopa kwa sababu alikuwa mkali maana nilivyoondoka kwake nilitoroka, ila Mfuko aliongea naye akamwambia nirudi atanipokea.
“Wakati nilivyofika, Mfuko alikuwa Gym na ilikuwa jioni hivyo nikamkuta yupo na Sharif. Niliongea nao kwa kuwaeleza kilichotokea upande wangu Sharif aliniambia nirudi atanisaidia mimi na mtoto wangu. Kwa kuwa nilishatafutiwa tiketi ya Dodoma nikaenda Dodoma kuwaeleza (ndugu) mwelekeo wangu hata ikitokea shida wajue nipo wapi.
“Nashukuru Mungu kweli baada ya muda nikarejea Bagamayo na Sharif ambaye kwangu ndiyo mlezi, baba na meneja wangu amekuwa akinielea kwa kila kitu hapa ndiyo anafanikisha.
“Lakini suala la malazi, kula yangu pamoja sehemu ambayo nalala kodi ya nyumba analipa yeye. Kwangu mimi hili ni jambo kubwa na hakuna chochote ambacho nimerudisha kwake.
Uliacha ngumi kwa kuona hazina faida sasa nini kimekufanya urudi tena kwenye ngumi?
(Baada ya kutafakari kwa muda, alijibu);
“Naweza sema wakati ule nilikuwa na utoto yaani sikujua nahitaji jambo gani la msingi kwa sababu upande mwingine najuta nafasi ambayo nilipoteza awali.
“Unajua yule Egine Kayange (bondia) ametokea hapa kwa Sharif na mimi ndiyo nilikuwa namfundisha ila sasa amepiga hatua kubwa hadi kufikia kuanza kujenga mji wake, lakini utoto ukanipoteza kabla ya kuamua kurudi upya.
“Angalia leo hii wapo kina Sara Alex ni mabondia ambao hawakuwepo wakati wangu. Hata rekodi yangu hawezi kuifikia, lakini leo Sara, Nasra Msami, Lelya Macho ni mabondia wakubwa kuliko mimi kwa upande wa wanawake.
“Lakini nashukuru nimerudi upya tayari mwaka jana nimecheza mapambano mawili ambayo yote nimeshinda kwa KO. Nataka ubingwa wao nimerudi upya.
Umewezaje kupata ufadhili wa kambi wa IBA, Russia kuelekea katika pambano lako mwezi ujao?
“Binafsi namshukuru meneja wangu Sharif pamoja na Juma Fadhil ndiyo wamefanikisha hili jambo baada ya kuomba mwaliko wa Chama cha Ngumi za Ridhaa Duniani (IBA) kupata kambi fupi ya kujifua kuelekea katika pambano langu litakalofanyika Zanzibar dhidi ya Sangeeta Birdi, mwezi ujao.
“Sasa najiandaa kusafiri kwenda Russia mapema mwezi ujao kabla ya kurejea kwa ajili ya pambano langu ambalo litakuwa la ubingwa wa mabara wa PST. Nataka kuwaambia mashabiki kuwa narudi upya kuendeleza rekodi yangu, lakini kukaa juu yao (wapinzani wake) kama nilivyoondoka.”
Unawaambia nini mabondia wenzako?
“Wanatakiwa kujua mwenyekiti wao nimerudi. Nataka kuchukua nafasi yangu na wale wote ambao walikuwa wanajiona wakali, basi wajue nawasubiri ndani ya ulingo kudhihirisha ubora wao.” Hivyo ndivyo anavyosema Rehema mwenye hadhi ya nyota moja na nusu.