KOCHA msaidizi wa timu ya taifa ya kikapu kwa wanawake wenye ya umri wa miaka 16, Nelious Mbungeni amesema mafunzo ya kikapu waliyoyatoa mkoani Singida yalimalizika kwa mafanikio.
Nelious aliliambia Mwanaspoti kwamba, wasichana 60 wenye umri wa kati ya miaka 10-18 walijitokeza kupata mafunzo katika Uwanja wa Karumeru uliopo wilayani Itigi.
“Idadi hiyo ni kubwa hasa kutokana na maeneo tuliyokuwa tunatoa mafunzo hayo,” alisema Nelious.
Alieleza kwamba lengo la mafunzo hayo ni kuwainua watoto wa kike ili waweze kucheza mchezo wa kikapu.
Kocha huyo alilipongeza Shirikisho la Kikapu Tanzania (TBF), Fravian Foundation na Giants of Africa kufanikisha mafunzo hayo.
Naye kamishina wa makocha wa TBF, Robert Manyerere alisema Nelious ni binti mdogo aliyeanza kufundisha mapema wenzake na kwamba akiendelea hivyo anaweza kufika mbali katika mchezo huo.
Hata hivyo kocha huyo alimshauri Nelious asiache kucheza kikapu kwani bado anahitajika kwenye timu ya taifa.