Jumuiya ya Waislamu yagonga mwamba kortini, Bakwata yaibuka kidedea

Arusha. Mahakama ya Rufani imeyatupa maombi ya Baraza la Wadhamini wa Jumuiya ya Waislam Tanzania ya kutaka Bodi ya Wadhamini ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), izuiwe kutekeleza hukumu ya mahakama ya Mahakama Kuu.

Jumuiya hiyo iliwasilisha maombi hayo namba 480/08 ya 2024 yaliyowasilishwa chini ya hati ya dharura ikitaka Bakwata izuiwe kuwaondoa kwa nguvu katika kiwanja namba 139 kilichopo Kitalu A Baruti kilichopo Musoma mkoani Mara.

Katika kiwanja hicho, ndipo ulipo msikiti unaoitwa Masjid Fuyrquan ambapo Bakwata ilifungua maombi namba 151 ya 2019 katika Baraza la Ardhi na Nyumba Musoma, ambapo mahakama hiyo ilitamka Bakwata ndio wamiliki halali.

Jumuiya hiyo ilikata rufaa Mahakama Kuu ikashindwa, na Bakwata ilipoanza kuwaondoa kwa nguvu wakisaidiwa na Polisi, ndipo Jumuiya hiyo ikakimbilia kortini kuomba wazuie kwa kuwa hawana amri halali ya mahakama ya kuwaondoa.

Hata hivyo, katika hukumu yake aliyoitoa Julai 24, 2024, Jaji Paul Ngwembe wa Mahakama ya Rufani aliyatupilia mbali maombi ya jumuiya hiyo.

Pande zote mbili zilikuwa zinakubali mmiliki wa mwanzo (original) wa kiwanja hicho alikuwa ni East Africa Muslim Welfare Society ambayo ilivunjwa mwaka 1968 na ndio chombo kilisimamia masuala yote ya Uislamu Afrika Mashariki.

Chombo hicho kilikuwa kikimiliki viwanja kikiwemo kiwanja hicho chenye mgogoro, ambapo baada ya chombo hicho kuvunjwa mwaka 1968, Bakwata ilidai kuwa mrithi wa mali zote za chombo hicho na jumuiya nayo ikidai ni mmiliki

Bakwata ilivyoshinda mwaka 2019

Ndipo Bakwata ikaamua kufungua maombi mbele ya Baraza la Ardhi na Nyumba Musoma ikidai kumiliki mali zilizokuwa za taasisi hiyo ya Afrika Mashariki kikiwamo kiwanja hicho, ambapo baraza hilo lilitoa uamuzi Desemba 8, 2019.

Katika uamuzi huo, baraza hilo la Ardhi na Nyumba lilimtangaza Bakwata kama mmiliki halali wa mali hizo ambapo Jumuiya ya Waislamu Tanzania haikuridhishwa na uamuzi huo na kuamua kufungua rufaa namba 4 ya 2023 na kushindwa.

Bado jumuiya hiyo haikuridishwa na uamuzi huo wa Mahakama Kuu uliotolewa Julai 24, 2023, ambapo Agosti 14 mwaka huohuo, ikafanikiwa kuwasilisha notisi ya kukata rufaa Mahakama ya Rufani na kuomba kupatiwa mwenendo na hukumu.

Sambamba na hilo, ikafungua maombi ya ardhi namba 66 ya 2023 ili kupata kibali cha kukata rufaa, ambao ulikuwa ni utaratibu wa kisheria wakati huo lakini utaratibu huo ulifutwa na mabadiliko ya sheria, hivyo ikayafuta maombi hayo.

Baada ya utaratibu wa kibali kufutwa na wao kuondoa maombi yao, Jumuiya hiyo inadai baadhi ya wanachama wa Bakwata walikwenda katika msikiti na kuandika maandishi ukutani kuwa tangu kuondolewa kwa maombi, wao ndio wamiliki.

Jumuiya ilivyokimbilia kortini

Katika maombi hayo ambayo yametupwa, jumuiya hiyo ikaeleza kuwa Bakwata ilianza kuwaondoa kwa nguvu bila amri yoyote halali.

Kupitia maombi yao ya kuizuia Bakwata isitekeleze hukumu ile ya Baraza la Ardhi na Nyumba ya mwaka 2012, na kupitia kiapo cha Atwarid Matambo, walieleza kuwa Machi 23, 2024, walimwandikia barua mkuu wa wilaya ili aingilie kati mgogoro huo.

Hata hivyo, mkuu huyo wa wilaya alisisitiza kuwa wanachama wa Bakwata ndiyo wako sahihi kwa kile wanachokifanya kwa kuwa ndio walioshinda kesi hivyo kuwataka jumuiya hiyo kuondoa katika eneo hilo.

Kutokana na uamuzi huo wa mkuu wa wilya, Matambo katika kiapo chake alidai kuwa Aprili 12, 2024, Katibu wa Bakwata Wilaya ya Musoma alikwenda katika msikiti huo na baadaye kuwafungulia kesi ya jinai yeye pamoja na wanachama wengine.

Kulingana na maelezo yake, yeye pamoja na wanachama wengine wa jumuiya walikamatwa na kushtakiwa kwa kosa la kufanya usumbufu katika kusanyiko la kidini kinyume na kifungu 126 cha kanuni ya adhabu.

Hivyo jumuiya hiyo ikaiomba mahakama itoe amri ya kuzuia utekelezaji wa hukumu iliyowapa ushindi Bakwata, ambayo iko mbioni kutekelezwa na kwamba tayari walishawasilisha notisi ya kukata rufaa kupinga hukumu ya Mahakama Kuu.

Katika ombi lao hilo, walisema kama amri ya kuzuia utekelezaji wa hukumu hiyo haitazuiwa na mahakama watapata hasara lakini katika kiapo kinzani cha Bakwata kilichosainiwa na Mikidadi Shada walikanusha maelezo ya jumuiya.

Bakwata ilivyoibuka kidedea

Baada ya kupitia kwa makini kumbukumbu za mahakama na hoja za mawakili, Jaji Ngwembe alieleza kuwa suala la kusuluhishwa katika ombi hilo la kuizuia Bakwata isitekeleze hukumu ni iwapo mwombaji amekidhi masharti ya kisheria.

Jaji amesema sheria inataka ili maombi kama haya yafanikiwe, mwombaji lazima atimize mahitaji yote yaliyoainishwa katika kanuni ndogo ya (4) ya Kanuni ya 11 ambayo inatoa kikomo cha muda wa siku 14 wa notisi.

Kulingana na Jaji Ngwembe, alisema mbali na yaliyomo katika kanuni hiyo ndogo iliyonukuliwa hapo juu, kwa usawa kanuni ndogo ya (5) ya kanuni hiyo ya 11 inatoa masharti ya ziada ya kutimizwa na Jaji akanukuu kifungu hicho.

“Hakuna amri ya kusitisha utekelezaji wa hukumu itatolewa chini ya kanuni hii isipokuwa kama Mahakama imeridhika kwamba hasara kubwa inaweza kusababishwa na mhusika kama amri ya kusimamishwa haitatolewa,” amesema.

Kwa mujibu wa Jaji Ngwembe, Kifungu (b) cha kanuni hiyo kinataka lazima dhamana iwe imetolewa na mwombaji kwa ajili ya utekelezaji unaostahili wa amri au amri ambayo hatimaye inaweza kuwa ya lazima kwake.

Jaji Ngwembe ameeleza katika suala hilo, hakuna utekelezaji unaoendelea au maombi yoyote yaliyofanywa na yanayosubiriwa mbele ya mahakama yoyote ya kisheria ya utekelezaji wa hukumu unatokana na kukaza hukumu.

“Nimeona kwenye hati ya kiapo ya mwombaji kuwa wanachodaiwa kufanya mawakala wa mlalamikiwa ni kuandika kwenye ukuta wa msikiti kuwa wao ndio wamiliki, majaribio ya kuwafukuza wanachama wa mwombaji na kuripoti polisi kuhusu baadhi ya tabia za wanachama wa mwombaji,” amefafanua Jaji.

Jaji amesema mahakama hiyo haiwezi kusitisha mashauri ya jinai mbele ya Mahakama ya Wilaya na vitendo vinavyolalamikiwa haviingii ndani ya uwanja wa Mahakama hiyo kuweza kushughulikia.

“Kando na hilo, amri ambayo utekelezaji wake unatafutwa kuzuiwa haujaambatanishwa katika maombi haya ya mapitio ya Mahakama,”amesema Jaji huku akinukuu maombi ya madai namba 424/ 2018 ya Septemba yanayofanana.

“Maombi ya aina hii yanaweza tu kuwasilishwa Mahakamani baada ya mwombaji kuwa na uhakika mchakato wa kutekeleza agizo hilo umeanzishwa na mwenye amri, na hii ni baada ya mwombaji kupewa taarifa ya utekelezaji uliokusudiwa na si kwa taarifa za tetesi,” alisisitiza Jaji Ngwembe.

“Kilichojiri katika kesi iliyotajwa, kinaonekana kufanana na maombi haya, ambapo mwombaji, aliwasilisha ombi hili wakati hakuna notisi yoyote ya utekelezaji wa hukumu wa mahakama unaokusudiwa,”aliongeza kusema Jaji Ngwembe.

“Baada ya kufikiria hivyo, maombi haya hayakubaliki, hayajakamilika na ni ya mapema kwa kukosa amri ya utekelezaji. Kwa hiyo, nayatupa maombi hay ana sitaamuru yeyote alipe gharama kwa sababu mzozo huo unatokana na dini,” alisema.

Related Posts