Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa ametoa mwezi mmoja (sawa na siku 30) kwa Wakurugenzi wa Halmashauri (DED) kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya shule 26 mpya za sekondari za bweni za wasichana.
Mpango wa ujenzi wa shule hizo za bweni za wasichana ulielezwa Machi 19, 2022 na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga kwa ajili ya masomo ya sayansi lengo likiwa kuhamasisha na kuongeza udahili kuanzia ngazi ya msingi, sekondari na vyuo vikuu.
Mchengerwa ametoa maagizo hayo jana Jumanne, Julai 30, 2024 kwa viongozi wa halmashauri wakati akipokea taarifa za ujenzi wa shule 26 za sekondari za wasichana za mikoa katika kikao cha tathmini ya ujenzi wa shule hizo kilichofanyika Ukumbi wa Arnautoglo jijini Dar es Salaam.
“Hakutakuwa na nyongeza ya muda katika kipindi ambacho tumekubaliana mkamilishe ujenzi wa miundombinu ya shule hizo, na sitasita kumchukulia hatua mkurugenzi yeyote atakayeshindwa kukamilisha ujenzi kwa mujibu wa makubaliano yetu,” amesema Mchengerwa.
Amesema alitegemea wakurugenzi watoe taarifa ya kukamilika kwa ujenzi wa shule hizo kwa asilimia 100 jambo ambalo halijatekelezeka, kwani alipokuwa kwenye ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan mkoani Rukwa aliahidi ndani ya mwezi mmoja ujenzi wa shule hizo utakuwa umekamilika.
Kikao hicho cha tathmini ya ujenzi wa shule 26 za sekondari za wasichana za mikoa, kimeudhuriwa na wakurugenzi wa halmashauri, maofisa elimu wa sekondari, wahandisi wa halmashauri na maofisa manunuzi wa halmashauri.
Hata hivyo, amesema wapo wakurugenzi ambao amewapatia wiki mbili, wiki tatu na wengine mwezi mmoja wa kuhakikisha wanakamilisha ujenzi wa sehemu zilizosalia katika shule hizo, isipokuwa mkurugenzi anayesimamia ujenzi wa shule ya Mkoa wa Rukwa ambaye amepewa miezi miwili.
Mbali na hilo, Mchengerwa amesema wanawategemea wakurugenzi hao katika usimamizi wa miradi mbalimbali inayolenga kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo, Kagurumjuli Titus amesema manispaa yake itakamilisha ujenzi wa miundombinu katika shule ya Mkoa wa Dar es Salaam kwani ameshawapatia fedha.
Naye, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Tunduma, Mariam Chaurembo akizungumza kwa niaba ya Mkoa wa Songwe, wamejipanga kukamilisha ujenzi wa sekondari ya Mkoa wa Songwe ndani ya mwezi mmoja.