Miaka 60 ya Muungano Tanzania kukutanisha wakuu wa mataifa saba Afrika

Dar es Salaam. Sherehe za maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar zinatarajiwa kuwakutanisha wakuu wa mataifa saba ya Afrika, watakaohudhuria tukio hilo kesho Ijumaa, Aprili 26, 2024.

Sherehe hizo zitakazofanyika katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, zitahudhuriwa pia na makamu wa rais wa mataifa mawili, Waziri wa Mambo ya Nje na wakuu wa taasisi mbalimbali za kimataifa.

Huu ni muongo wa sita, tangu Tanganyika na Zanzibar ziungane na kuunda Tanzania, Aprili 26, 1964, chini ya Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume.

Hata hivyo, kufikisha miaka 60 kunaufanya muungano huo, uwe uliodumu zaidi miongoni mwa mataifa ya Afrika yaliyowahi kuungana.

Mbali na Tanganyika na Zanzibar, Ghana na Guinea ziliwahi kuungana baada ya mkutano wa watu wa Afrika na mwaka 1959, muungano huo ulitangazwa kuwa utatambulika kama Umoja wa Dola za Kiafrika.

Waziri wa Mambo ya Nje ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba akizungumza na Rais wa Kenya, William Ruto baada ya kumpokea Dar es Salaam leo Aprili 25, 2024

Mambo yalinoga zaidi mwaka 1961, taifa la Mali lilipojiunga na umoja huo na kuufanya uwe na mataifa matatu. Lakini furaha hiyo ilidumu kwa mwaka mmoja baada ya 1962, muungano huo kuvunjika kutokana na vita baridi.

Senegal na Gambia nazo ziliungana mwaka 1981 na kuunda Senegambia iliyodumu hadi mwaka 1989 kisha kuvunjika.

Taarifa kuhusu wakuu wa nchi hao watakaohudhuria sherehe hizo, imetolewa leo Alhamisi, Aprili 25, 2024 na Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Mobhare Matinyi.

Amewataja wakuu hao wa nchi watakaohudhuria ni Rais Azali Assoumani (Comoro), Félix Tshisekedi (Jamhuri ya Demokrasia ya Congo), Évariste Ndayishimiye (Burundi) na Hakainde Hichilema (Zambia).

Wengine ni Hassan Sheikh Mohamud (Jamhuri ya Somalia), William Ruto (Jamhuri ya Kenya) na Nangolo Mbumba (Namibia).

Kwa upande wa Makamu wa Rais watakaohudhuria, amemtaja Saulos Chilima wa Malawi na Jessica Alupo wa Uganda.

Kwa mujibu wa Matinyi, Waziri Mkuu wa Msumbiji, Adriano Afonso Maleiane naye ni miongoni mwa viongozi wakuu wa nchi za Afrika atakayehudhuria.

Mbali na hao, Waziri wa Nchi anayeshughulikia Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kikanda wa Rwanda, Jenerali mstaafu James Kabarebe na Katibu wa Mambo ya Nje wa chama cha ZANU PF cha Zimbabwe, Balozi Simbarashe Mumbengegwi naye atahudhuria.

Katika sherehe hizo pia, Matinyi amesema Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Dk Akinwumi Adesina anatarajiwa kuhudhuria.

“Hivi sasa tunaendelea kuwapokea kwa kuwa wote wamethibitisha kuhudhuria,” amesema Matinyi.

Related Posts