Dk Ndugulile ataja maeneo manne kukabili uhaba watumishi wa afya

Dar es Salaam. Mbunge wa Kigamboni, Dk Faustine Ndugulile ameshauri mambo manne yanayoweza kusaidia kupunguza uhaba wa wataalamu katika maeneo mbalimbali ya kutolea huduma za afya nchini Tanzania.Maeneo aliyoshauri ni kutumia mwongozo wa wataalamu kujitolea, kutoa kipaumbele cha ajira kwa waliojitolea, matumizi ya sayansi na teknolojia na kuanzisha kada mpya ya ‘family medicine’.Ametoa ushauri huo wakati ambao nchi inakabiliwa na uhaba wa watumishi katika ngazi ya vituo vya afya kwa takribani asilimia 60.Dk Ndugulile ametoa kauli hiyo katika kilele cha maadhimisho ya kumbukizi ya Hayati Benjamin Mkapa yaliyoandaliwa na Taasisi ya Benjamin Mkapa (BMF) na kufanyika leo Jumatano, Julai 31, 2024 jijini Dar es Salaam huku Rais Samia Suluhu Hassan akiwa ndiye mgeni rasmi.Dk Ndugulile amesema kama nchi imekuwa ikifanya uzalishaji wa rasilimali watu wengi lakini hawajaajiriwa na upo mwongozo wa watumishi wa afya kujitolea jambo ambalo ametaka lifanyike.“Tutumie mwongozo huu, tuwatumie wale vijana wakienda kufanya kazi watakuwa wanapata ujuzi, kuzalisha na fedha hizo zitaweza kuwasaidia kujikimu,” amesema Dk Ndugulile.Wakati matumizi ya mwongozo kwa watumishi hao ukitumika pia alitaka wale wanaokuwa tayari kujitolea kupewa kipaumbele ajira zinapotolewa tofauti na sasa.“Mfumo wa sasa si mzuri sana, mtu anakwenda kujitolea Lindi ajira zinapokuja yeye hapati fursa waliokuja wapya wanapata fursa na hawataki kwenda wengine waliokokuwa wakijotolea,” amesema Dk Ndugulile.Hayo yaende sambamba na matumizi ya sayansi na teknolojia kwani dunia inazungumzia masuala kama akili mnemba (Artificial intelligence), ubunifu na uvumbuzi huweza kusaidia,” amesema.Amesema kama nchi imefanya uwekezaji katika kununua mashine za kufanyia vipimo vya kidijitali (digital X–Ray) ambayo inaweza kufanya picha inayopigwa Tandahimba kusomwa Dar es Salaam na kurudishwa ilikotoka jambo ambalo linaonyesha namna gani njia hiyo ikitumika vyema huweza kusaidia.Eneo la tatu aliloshauri ni kuangalia namna ya kuja na kada mpya kwani dunia ya sasa inaongelea afya ya msingi na ushirikishaji wa jamii.“Sasa nilitaka tutafakari jambo lingine, sasahivi tunashukuru Serikali inasomesha wataalamu na madaktari bingwa lakini tufikirie namna ya kuanzisha family medicine, hawa ni wataalamu wa afya ambao wamesomea mambo mengi wanaoweza kuisaidia sekta ya afya,” amesema.Amesema wataalamu hao wanaweza kuwa wamesomea afya ya mama na mtoto, wanajua afya za wazee na kila kitu hivyo uwepo wao utachocchea utoaji wa huduma.“Suala la Rasimilami watu si suala la sekta ya afya pekee hivyo ni vyema kuangalia mtiririko mzima, mafunzo, mipango, namna gani tunaajiri na jinsi gani tunaweza kuwapa motisha, hivyo sekta mbalimbali za afya lazima zishiriki kama ilivyokuwa kwa taasisi ya Benjamin Mkapa,” amesema Dk Ndugulile.Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Mary O’Neill amesema menejimenti ya BMF inayo dhamira ya kuhakikisha kazi ya Hayati Mkapa inadumishwa na kuzifikia jamii nyingi kwa huduma zinazohitajika kwa Tanzania Bara na Zanzibar.Alitumia nafasi hiyo kuipongeza Serikali kwa dhamira endelevu iliyonayo kwa kufanya uwekezaji katika rasilimali watu, hasa kwa wanawake na wasichana.Amesema kupitia mtaji wa watu ulioendelezwa vizuri ndiyo nchi zinaweza kufikia ukuaji endelevu wa uchumi na shirikishi na kwa ustawi wa jumla wa watu wake wote.“Tunahimiza Serikali kufanya kazi kwa karibu zaidi na sekta binafsi ili washiriki kikamilifu katika maendeleo ya rasilimali watu na kuimarisha utoaji wa huduma bora za afya nchini kote.Hii itajumuisha kusaidia na kufanya kazi na vituo vya afya vya kibinafsi na vya kidini na watoa huduma ili kusaidia kujaza mapengo, na kufanya kazi na kampuni za kibinafsi ili kuboresha ufikiaji wa huduma,” amesema.Amesema Tanzania imepiga hatua kubwa kuelekea kufikiwa kwa malengo kadhaa, hususan lengo la tatu la maendeleo endelevu kuhusu afya na maendeleo endelevu lengo la tano la usawa wa kijinsia.

Related Posts