Serikali yajitosa kukabili changamoto ya wataalamu wa nishati jadidifu

Hai. Katika kukabiliana na changamoto ya uhaba wa wataalamu wa nishati jadidifu Tanzania,  Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kupitia mradi wa kujenga ujuzi na kuimarisha ushirikiano wa Afrika Mashariki (EASTRIP), imejenga kituo cha kisasa cha kikanda cha umahiri kiitwacho Kikuletwa.

Kituo hicho kitakuwa kinatoa mafunzo kwa wataalamu wa nishati hiyo na ujenzi wake umegharimu zaidi ya Sh37.5 bilioni.

Wataalamu hao ni pamoja na wale wanaobadili mifumo ya magari ili kutumia gesi kama mbadala wa nishati ya petroli na dizeli. Akizungumza baada ya kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa Ndaki ya Kikuletwa ya Chuo cha Ufundi Arusha (ATC), iliyoko Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Waziri wa Elimu, Sayansi, na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema ndaki hiyo ni miongoni mwa miradi minne mikubwa inayotekelezwa nchini kwa gharama ya zaidi ya Sh187 bilioni.

Mbali na mambo mengine, Profesa Mkenda amesema bado kuna tatizo kubwa la ukosefu wa mafundi wa magari ya kisasa nchini.

Amesema magari hayo yanapoingia nchini na kukutana na changamoto za kiufundi, inakuwa vigumu kupata mafundi wenye ujuzi wa kuyatengeneza.

“Tujenge mahusiano mazuri na makampuni ya magari ya nje kupitia vyuo vyetu hivi vya ufundi  ili tubadilishe uzoefu, ili watu wetu nao sasa wawe wabobevu katika utengenezaji wa magari haya, tusijifungie milango ikiwezekana waje kwetu nasi wanafunzi wetu waende huko kujifunza,”amesema Profesa Mkenda.

Hivyo ametoa wito kwa vyuo vya ufundi nchini,  kujenga uhusiano na kampuni za magari kutoka nje ya Tanzania kupitia vyuo vya ufundi vya nchi zao kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kuhakikisha wanafunzi wa Tanzania wanapata ujuzi wa kutengeneza magari hayo ya kisasa.

Pamoja na hayo, Profesa Mkenda amesema kuzalishwa kwa wataalamu hao kutaisaidia Tanzania na wadau wengine kukabiliana na changamoto ya uhaba wa mafundi wa magari ya kisasa.

“Tunaishukuru serikali kwa kutoa fedha hizi na katika mradi huu wa nishati jadidifu, imetoa Sh37.5 bilioni kwa ajili ya chuo hiki cha Kikuletwa na utashirikisha nchi tatu, ikiwemo Kenya, Tanzania na Shirikisho la Jamhuri ya Ethiopia,” amesema Profesa Mkenda.

Naye, Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Utawala ya Chuo cha Ufundi Arusha (ATC), Francis Kisangire ameishukuru serikali kwa kuhakikisha wataalamu wabobezi wanazalishwa katika ndaki hiyo.

Mkuu wa Chuo cha ATC, Profesa Mussa Chacha amesema uwepo wa chuo hicho utaongeza umahiri katika kuzalisha wataalamu wa masuala mbalimbali ya ufundi nchini.

Related Posts