KIPA mkongwe kwenye Ligi Kuu Bara, Shaban Kado amesema maandalizi yanayofanywa na Pamba Jiji ni ishara ya timu hiyo kutaka kufanya vizuri kwenye michuano hiyo na kutotaka mazoea ya timu zinazopanda daraja kushuka mwishoni mwa msimu.
Kado ambaye ni msimu wake wa pili Pamba Jiji baada ya kuipandisha Ligi Kuu na kuongezewa mwaka mmoja, alisema timu mpya inapopanda Ligi Kuu inakabiliwa na presha lakini akawatoa mashabiki wasiwasi kwamba uwepo wa wachezaji wazoefu utasaidia kuwapa mbinu nyota wapya.
Alisema maandalizi waliyofanya jijini Mwanza na Morogoro chini ya Kocha Mkuu, Goran Kopunovic ni ya hatari na kikosi hicho kitawashangaza watu wengi kwenye Ligi Kuu kwa soka la kisasa na la matokeo ya ushindi.
“Timu haikuwa ligi kuu kwa muda mrefu kwahiyo kunakuwa na presha fulani lakini tunashukuru Mungu wachezaji wengi ni wazoefu na vijana wachache kwahiyo tunapeana uzoefu kuondoa presha na wasiwasi ili tufanye vizuri.
“Naviona vitu vingi vizuri na kama tutakopi mapema na wenzangu naamini tutawashangaza watu kwenye ligi kwa namna timu itakavyokuwa inacheza. Mashabiki waendelee kutusapoti na wategemee mpira mzuri na wenye matokeo,” alisema Kado.
Kocha wa makipa wa Pamba Jiji, Razack Siwa alisema kikosi chao kimesheheni wachezaji wengi vijana ambao wanapokea vizuri maelekezo ya benchi la ufundi, huku akiahidi kutengeneza makipa wazuri watakaoisaidia kupata matokeo mazuri.
“Mimi napenda mtu mwenye bidi na wengi nilionao wanajituma nategemea kupata makipa wazuri kwa sababu wanafanyia kazi maelekezo ninayowapa. Kipa akiweza kujituma, kujisahihisha anapokosea na kuheshimu ninachokifanya ni rahisi kumsaidia kuwa kipa bora,” alisema Siwa.