Mwanza. Upelelezi wa shauri la mauaji linalomkabili Mchungaji wa Kanisa la Tanzania Assembly of God (T.A.G) lililopo Buhongwa jijini Mwanza, Ernest George (37) haujakamilika.
Akisoma shtaka hilo lenye kesi namba 19830/2024 leo Jumatano Julai 31, 2024 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza mbele ya Hakimu wa mahakama hiyo, Stella Kiama, Wakili wa Serikali, Martha Mwandenya amesema bado wanaendelea na upelelezi na hivyo ameiomba mahakama kupanga tarehe nyingine ya kusikiliza shauri hilo.
Baada ya wakili huyo kusema hivyo, Hakimu Kiama ameahirisha shauri hilo hadi Agosti 14, 2024 litakapoitwa kwa ajili ya kutajwa.
Hata hivyo, mshtakiwa ameomba hati ya mashtaka kwa ajili ya kusikilizwa upya kesi yake na Hakimu Kiama amemwambia hawezi kupewa hati hiyo kwa kuwa kesi hiyo haiwezi kusikilizwa katika Mahakama hiyo.
“Charge Sheet (hati ya mashtaka) utapewa utaratibu wa kuzisoma hoja za awali zikishakamilika na hatujafikia hiyo stage (hatua hiyo)..lakini pia Mahakama haina mamlaka ya kusikiliza shauri lako,” amesema hakimu huyo.
Amemueleza mshtakiwa kinachoendelea sasa mahakamani hapo ni taratibu za kutaja shauri na atapewa taarifa zote zinazohusiana na kesi hiyo baada ya kuhamishiwa Mahakama Kuu ambayo ndiyo ina uwezo wa kuisikiliza.
Katika shauri hilo ambalo lilitajwa kwa mara ya kwanza Julai 17, mwaka huu, Wakili wa Serikali, Evance Kaiser aliiambia Mahakama hiyo kuwa, mshtakiwa alitenda kosa hilo kinyume na kifungu namba 196 na 197 cha kanuni ya adhabu namba 16 ya marejeo ya mwaka 2012.