KOCHA Mkuu wa Dodoma Jiji, Mecky Maxime amesema anaendelea kukisuka kikosi chake kuwa bora na kutoa ushindani mkubwa msimu ujao, huku akitaka kuona kila mchezaji ndani ya kikosi hicho anakuwa staa.
Katika maandalizi ya timu hiyo kuelekea msimu ujao, tayari imecheza mechi tatu za kirafiki ikianza na Pamba na kushinda bao 1-0, ikaichapa Singida Black Stars mabao 2-1 na juzi iliikanda Namungo kwa mabao 3-0.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mexime alisema anafurahishwa na ubora wa wachezaji wake namna ambavyo wanapambana kumshawishi ili aweze kuwatumia kikosi cha kwanza.
“Hadi sasa nimegundua nina kikosi kizuri, kilichobaki ni kuwajenga wachezaji wangu waweze kuwa timamu ili kucheza mechi kwa dakika zote 90 na kutoa changamoto kwa wapinzani,” alisema na kuongeza:
“Ukuta na washambuliaji wote wapo vizuri na kila mchezaji anapambana kuonyesha kile alichonacho, hii inanipa nguvu kuamini kuwa nitakuwa na msimu mzuri licha ya kujipa muda zaidi wa kuendelea kuboresha timu.”
Mexime alisema Dodoma Jiji itakuwa timu shindani na anaamini atakuwa na kikosi ambacho kila mchezaji ni muhimu kutokana na namna anavyoliandaa jeshi lake kwa kutoa nafasi kwa kwa wote.
“Siwezi kuwa na mchezaji ambaye asipokuwepo timu inayumba, naandaa timu ambayo kila mchezaji atakuwa na umuhimu kikosini, hili nimeshaliona na nina matumaini makubwa kuwa kila mchezaji atakuwa staa kulingana na mchango wake,” alisema.