Kocha Red Arrows aikubali Yanga

KOCHA Mkuu wa Red Arrows ya Zambia, Chisi Mbewe amesema, baada ya kupata mualiko wa kucheza na Yanga katika kilele cha ‘Wiki ya Mwananchi’, imekuwa ni jambo nzuri kwao, kwani wanaenda kukutana na timu imara itakayowapa changamoto mpya.

Timu hiyo ambayo ni mabingwa wa Ligi Kuu ya Zambia (ZPL), itawasili muda wowote kuanzia sasa kwa ajili ya kusherehesha mchezo huo muhimu unaosubiriwa kwa hamu utakaopigwa Jumapili ya Agosti 4, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

“Tunaenda kukutana na timu nzuri ambayo itakuwa ni kipimo kizuri kwetu hasa wakati huu ambao tuko katika maandalizi ya msimu ujao, isingekuwa rahisi kukataa mualiko waliotupatia kwani tuliamini wao pia ni mabingwa na watatupa ushindani.”

Mbewe aliongeza, anaiheshimu Yanga kwa sababu ni timu nzuri na yenye wachezaji bora hivyo anakuja na kikosi kamili kwani mchezo huo anauchulia kwa uzito mkubwa, huku akiainisha lengo lake ni kuendelea kupata maandalizi mazuri ya msimu ujao.

“Kila mmoja anatambua ukubwa na ubora wa Yanga hivyo tunaweza kuuita mchezo wa mabingwa, utaendelea kutupa taswira kwa msimu ujao na namna ya kuangalia mapungufu na jinsi ya kuyarekebisha kama ilivyokuwa pia kwenye michuano ya Kagame.”

Wakati kikosi hicho kikitarajiwa kutua nchini muda wowote kwa ajili ya mchezo huo, ila tayari kimeinasa saini ya winga Mkongomani, Emmanuel Bola Lobota aliyekuwa anawindwa na Yanga kwa mkopo wa mwaka mmoja akitokea Singida Black Stars.

Mbali na ubingwa wa Zambia, ila Red Arrows ni mabingwa wa Kombe la ABSA 2024, huku ikichukua pia Kombe la Kagame mwaka huu jijini Dar es Salaam, baada ya kuifunga APR ya Rwanda kwa penalti 10-9, kufuatia sare ya bao 1-1, ndani ya dakika 120.

Related Posts