SAKATA LA KIBU: Simba yatoa sharti jipya, yataja bei

Dar es Salaam. Simba imetoa sharti gumu kwa mchezaji wake Kibu Denis na Kristiansund BK inayomhitaji ili imruhusu mshambuliaji huyo kujiunga na timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya Norway.

Sharti hilo ni kuitaka Kristiansund BK kulipa kiasi cha Dola 1 milioni (Sh 2.7 bilioni) ili kumnunua moja kwa moja mshambuliaji huyo vinginevyo haitokuwa tayari kumuachia kwa dau la fedha chini ya hilo.

Mmoja wa viongozi wa Simba ameiambia Mwananchi kuwa wamefikia uamuzi huo ili kutoa fundisho kwa wachezaji na klabu za soka kuheshimu mikataba kama miongozo ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (Fifa) inavyofafanua.

“Kuna makosa matatu makubwa ambayo yamefanyika katika suala hilo la Kibu (Denis) ambayo Simba tukisema tusichukue hatua hatuwezi kusaidia soka hasa katika suala la kuheshimu mikataba kwa wachezaji na timu. Kosa la kwanza ni mchezaji kuidanganya klabu na kutorika akijua kabisa ana mkataba tena wa muda mrefu ambao ametoka kuusaini.

“Kosa la pili limefanywa na hiyo timu ya Norway la kufanya mazungumzo kinyemela na mchezaji wa timu nyingine ambaye bado ana mkataba huku ikiwa kinyume na kanuni za Fifa na kosa la tatu ni mchezaji kuharibu taswira ya klabu kwa kusema uongo kuwa inafahamu7 sababu ya kutokuwepo kambini huku ikiwa kinyume chake,” amesema kiongozi huyo.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo, Simba imetoa sharti kwa klabu hiyo ya Norway kuvunja mkataba kwa dau la Dola 1 milioni na kinyume na hapo itaishtaki.

“Tumeona na kusikia upande wa mchezaji unajaribu kutuomba na kutushawishi tumuuze kwenda Norway lakini kwa dau wanalotaka wao jambo ambalo sio sawa na linazidi kumuweka huyo mchezaji matatizoni. Msimamo wa klabu haujabadilika ambao ni kuitaka hiyo timu imnunue moja kwa moja mchezaji kwa dau la Dola 1 milioni na sio kufanya majaribio ya mwezi mzima kama wanavyotaka.

“Ikishindikana tutaishtaki hiyo timu kwa Fifa kwa kosa la kumtorosha mchezaji wetu na uthibitisho wote tunao ambao ni barua ya kuomba radhi ambayo Kristiansund wametuandikia na pia ya ofa waliyoileta mezani lakini pia uthibitisho wa mchezaji mwenyewe,” amefafanua kiongozi huyo.

Meneja wa Kibu Denis, Carlos Sylivester alinukuliwa akisema kuwa upande wao watakaa na Simba ili kutafuta suluhisho la shauri hilo lililojitokeza.

“Kibu anapaswa kufahamu, hakuna namna anaweza kuikwepa Simba kwani ana mkataba nao kama kuna jambo lolote ni vizuri kukaa mezani azungumze na viongozi wake kusudi jambo hili lifikie kikomo,” alinukuliwa Sylivester.

Sakata la Kibu lilianza mapema mwanzoni mwa mwezi uliopita baada ya mchezaji huyo kusaini mkataba mpya wa miaka mitatu kuichezea timu hiyo, kuomba ruhusa na kutimkia Marekani kwa ajili ya mapumziko.

Mara baada ya muda wake wa ruhusa ya mapumziko kumalizika, Kibu hakuungana na wenzake waliokuwa kambini Misri kwa kile kilichotajwa kuwa hati yake ya kusafiria imeisha muda wake na licha ya kupewa hati mpya hakuwa tayari kwa safari akiwaeleza viongozi kuwa atakwenda huko atakaporejea kutoka Kigoma alikokwenda kuiona familia.

Simba ikamtaka kuwasilisha hati ya kusafiria ili iandaliwe kwa kuwekwa visa ya kuingia Misri, lakini bado akaibua jipya akidai ameisahau Dar na hakuna mtu wa kuweza kuingia  nyumbani kwake jambo lililoifanya Simba kukwamia hapo.

Lakini siku chache baadaye ilibainika kuwa mchezaji huyo ameondoka kinyemela kwenda Norway baada ya kupata mualiko na Kristiansund wa kufanya majaribio ya mwezi mmoja.

Related Posts