May Day ni ya wafanyakazi wastaafu je?

Siku ya kwanza ya Mei, wafanyakazi nchini wanajiunga na wafanyakazi wengine duniani kuadhimisha sikukuu yao ya ‘May Day.’ Inaelezwa kuwa ni kumbukumbu ya wafanyakazi kukata minyororo ya uonevu na kujikomboa kutoka kwa waajiri wao waliokuwa wanawaonea. Kwa Tanzagiza wafanyakazi wanasherehekea tu kupata sare mpya na kuandamana. Labda mara hii kikokotozi kitachapa lapa!

Ni Sikukuu ya Wafanyakazi. Mstaafu wetu anasema zamani wakati wanaijenga nchi hii kwa damu na jasho lao walizoeshwa, na kuzoea, kuisubiri siku hii muhimu kwa hamu kubwa kwa sababu ilikuwa ni siku ambayo aliyekuwa Baba wa Taifa angetangaza ongezeko la kima cha chini cha mshahara na wafanyakazi wote walitoka kwenye mkutano husika wakifurahia ongezeko hilo, hata kama ilikuwa ni la shilingi 280, rudia hapo mia mbili themanini! Liliwatosha.

Mstaafu wetu anasema wafanyakazi nchini wakaaminishwa na kuamini kwamba May Day ni kuongezwa mshahara na siyo kuandamana tu na kujipatia sare mpya za May Day. Ndivyo ilivyokuwa. Hata baada ya vita vya Kagera Watanzania walipotakiwa kukaza mikanda kwa miezi 18 maana nchi ilikuwa inapita kwenye kipindi kigumu kiuchumi, bado May Day iliyofuata mishahara ilipandishwa, japo kwa shilingi 120, rudia tena hapo, kwa shilingi mia moja ishirini !

Mstaafu wetu anasikitika sana May Day za miaka hii zimekuwa za wafanyakazi kuvaa sare mpya tu za sikukuu na mikutano tu (ambayo mjukuu mmoja wa Mstaafu anaiita ni ‘blah blah tu’, maneno yake mjukuu, sio ya Mstaafu!).

Anasema kama ni kweli May Day ni kumbukumbu ya waajiriwa kukata minyororo ya uoenevu ya waajiri wao, basi kikokotoo na pensheni ya ‘Laki si Pesa’ vingeishachapa lapa!

Mstaafu anasikitika sana utamaduni huu wa kutumia May Day kutangaza nyongeza ya mishahara kwa wafanyakazi imeyeyushwa na wafanyakazi wanaishia kuambiwa tu ‘tuna jambo letu’ na likachukua muda kutekelezwa na linapotekelezwa linakuwa sio matumaini waliyotegemea mno kwa hamu! Sana sana yanaishia kuwa kama yale yale ya nyongeza ya mishahara kwa shilingi 120 kwa mwezi! Sisi ilitutosha, nyinyi?

Kwa hakika, inasikitisha mno May Day imeishia kuwa siku ya kushindana sare na hata mabango ya malalamiko ya wafanyakazi yanayoandikwa humo yanaishia pale pale kiwanjani! Yangekuwa yanafanyiwa kazi, mishahara na pensheni vingekuwa vimepanda zamani kwa viwango vya kuheshimika na vya kueleweka.

Hilo ni moja, Mstaafu wetu anasema kubwa ni hili la kuona hapa nyumbani ukiisha staafu na kuwa Mstaafu, May Day haikuhusu tena, wewe sio mfanyakazi maana May Day ni ya wafanyakazi sio wastaafu. Ndio maana hata siku moja hutaona wastaafu wakiwa wamevaa sare zao kuukuu za ‘kaa chonjo saa mbaya’ walizovaa enzi hizo wameitwa na kujumuishwa kwenye maandamano ya May Day! Nani ana haja nao?
Mstaafu anasikitika sana kuona hivi vyama rundo vya wafanyakazi hakuna hata kimoja ambacho kimeona umuhimu wa kuwaita wastaafu kutoka chama chao waandamane kwenye May Day maana walikuwa waajiriwa wa jana na wafanyakazi wanaondamana kwenye May Day ni wastaafu watarajiwa! Kweli hawalioni hili, huku ‘Laki si Pesa’ na kikokotoo vikiwasubiri?

Wataweza na wao kukaa miaka 19 wakibembeleza kuongezwa pensheni yao ya ‘Laki si Pesa’ wakati ni haki yao? Wanashindwaje kuanza kulifanyia kazi sasa wakati bado wakiwa wafanyakazi wanaoweza kuandamana May Day na sio kusubiri wakiwa wastaafu na walazimike kukaa miaka 19, kama wazazi wao, wakisubiri nyongeza ya pensheni?

Mstaafu wetu anaona sasa wakati umefika kwa hawa viongozi wa kisasa wa vyama rundo hivi vya wafanyakazi kuwaongoza wafanyakazi wao kubeba mabango yanayoonekana wazi kabisa kwenye maandamano ya May Day ya kupiga vita kikokotoo kwenye mafao yao kichape lapa. Wasiishie kwenye kuandaa sare tu za kuwapendezesha wafanyakazi wao. May Day ni zaidi ya hivyo. Maisha ni zaidi ya kuteuliwa!

Waone kuwa haingii akilini mtu kukatwa mshahara wake kwa ajili ya akiba ya uzeeni halafu ukifika wakati wa kustaafu waheshimiwa wanakuamulia kuwa wasikupe mafao yako yote uangalie ustaarabu mwingine, ila wanakuamulia kukupa kiduchu kiduchu maana wakikupa zote ati utazitumia vibaya! Yaani umeajiriwa na kukatwa kodi miaka 40 ya ajira na akili yako, lakini ukistaafu na kupaswa kupewa chako, ghafla huna akili na utayatumia vibaya mafao yako!

Wafanyakazi anzieni hilo kisha la ‘laki si pesa’ ambayo ina miaka 19 sasa imeganda pale pale kama lile sanamu la askari! Wastaafu wamestaafu lakini wanaamini kuwa bado wana haki ya kutetewa kuongezwa pensheni yao ya ‘laki si pesa’ ambayo inapiga ‘makitaimu’ palepale kama ile sanamu ya askari kwa miaka 19 sasa, pale Mtaa wa Samora. Wastaafu wasingoje kukaa vifua wazi pale Daraja la Selanda.

Related Posts