Dar es Salaam. Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limetangaza nafasi za kuandikishwa jeshini kwa vijana wa Kitanzania wenye elimu ya kidato cha nne na kidato cha sita na wasiozidi miaka 25.
Uandikishwaji huo utahusisha pia vijana waliopo katika makambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (Operesheni Jenerali Venance Mabeyo) na waliomaliza mkataba ambao wamefanya mafunzo ya JKT kwa Mujibu wa Sheria na kwa Mkataba wa kujitolea.
Hiyo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na JWTZ kupitia Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano Makao Makuu Jeshini, Luteni Kanali Gaudentius Ilonda.
Taarifa hiyo ya nafasi za jeshi inakuja ikiwa ni siku chache tangu Julai 23 mwaka huu watu 2,068 kuitwa katika usaili kwa ajili ya ajira ndani ya Jeshi la Polisi. Usaili huo ulianza Julai 29 na unatarajiwa kukamilika Agosti mosi mwaka huu.
Kwa mujibu wa tangazo la JWTZ, waombaji wanatakiwa kuwa sifa tofauti ikiwemo waliomaliza mkataba na Jeshi la Kujenga Taifa au ambao wapo huko.
Pia, waombaji wanatakiwa kuwa raia wa Tanzania, umri usiozidi miaka 25, wawe na afya nzuri na akili timamu.
“Mwenye tabia na nidhamu nzuri, hajapatikana na hatia ya makosa ya jinai mahakamani na kufungwa, wawe na cheti halisi cha kuzaliwa, wawe na vyeti vya shule, awe hajatumikia Jeshi la Polisi, Magereza, Chuo cha Mafunzo au Kikosi Maalumu cha kuzuia Magendo,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Pia, muombaji anatakiwa kuwa amehitimu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa Mkataba wa kujitolea miaka miwili (2) au mafunzo ya Mujibu wa Sheria na kutunukiwa cheti.
Ili kutuma maombi hayo, kwa waliopo katika makambi ya JKT ‘Operesheni Jenerali Venance Mabeyo’ taratibu zao zinaratibiwa na Makao Makuu ya Jeshi huku waliopo makambi ya JKT, maombi yao yaandikwe kwa mkono na kuwasilishwa Makao Makuu ya Jeshi Dodoma kuanzia Agosti Mosi hadi Agosti 14, 2024 mwaka huu.
Maombi hayo yanatakiwa kuambatanishwa na nakala ya kitambusho cha Taifa au namba ya NIDA, nakala ya cheti cha kuzaliwa, nakala za vyeti vya shule, nakala ya cheti cha JKT na namba ya simu ya mkononi ya mwombaji.