Madereva magari ya Serikali wanaoendesha kibabe barabarani sasa kukiona

Geita. Jeshi la Polisi mkoani Geita kupitia kitengo cha Usalama Barabarani, limewatahadharisha madereva wanaoendesha magari ya Serikali kuacha kutumia mwavuli wa kuwa madereva wa Serikali kama kisingizio cha kufanya makosa barabarani.

Hii ni baada ya kuonekana kuwa baadhi ya madereva hao hawazingatii sheria za usalama barabarani, wakitegemea kwamba utetezi wa kuwa wao ni madereva wa Serikali utawaepusha na adhabu.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha Usalama Barabarani Mkoani Geita, Jacob Aloyce, utetezi huo hautapokelewa tena na badala yake, madereva watakaopatikana na hatia watanyang’anywa leseni na kufikishwa mahakamani.

Hatua hii imelenga kutoa fundisho kwa madereva wengine, huku sheria ikitekelezwa kwa usawa bila kujali cheo au nafasi ya dereva husika.

Aloyce ametoa onyo hilo leo Jumanne Julai 31, 2024, wakati wa mafunzo maalumu kwa madereva wa magari ya Serikali yaliyolenga kuwakumbusha kuhusu sheria za usalama barabarani.

Ameyataja makosa yanayoongoza kutendwa na madereva hao ni pamoja na mwendokasi, kupita magari mengine sehemu zisizoruhusiwa, na kutozingatia alama za barabarani hususan kwenye vivuko vya watembea kwa miguu.

“Hapo stendi aligongwa mtu kwenye ‘Zebra cross’, kifungu cha 65 cha sheria za usalama barabarani kiko wazi, lakini ninyi hamsimamii na mnagonga watu. Mnatumia utetezi kuwa wewe ni dereva wa Serikali. Niwaambie kuanzia leo sitawavumilia wala kuwasikiliza, nitakufungia leseni na nitamwambia mwajiri wako asikupe gari,” amesema Jacob.

Mafunzo hayo ya siku nne yaliyoandaliwa na Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Geita (GGML) kwa kushirikiana na Kitengo cha Usalama Barabarani, yanalenga kuwakumbusha madereva sheria za usalama barabarani hususan katika barabara za kuingia mgodini na uendeshaji unaohitaji umakini mkubwa.

Meneja wa Idara ya Ulinzi kutoka GGML, Silivester Mgaba amesema ajali nyingi zimekuwa zikihusisha pia barabara za mgodini na kwamba, mafunzo hayo sasa yanalenga kuzuia ajali zisizo za lazima kwa kuhakikisha madereva wanazingatia sheria na taratibu za usalama barabarani.

Chrispin Christian, dereva kutoka Jeshi la Uhamiaji, amesema mafunzo hayo yatawasaidia siyo tu kutii sheria za barabarani, bali pia kujua sheria za kuendesha magari kwenye maeneo ya migodi.

Kwa Tanzania, ajali za barabarani na takwimu zinaonesha katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2019 hadi Mei 2024, ajali 10,093 zilisababisha vifo vya watu 7,639 na majeruhi 12,663.

Katika kipindi hicho pia, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba aliwahi kusema kwenye moja ya mkutano wake na viongozi wa polisi Kitengo cha Usalama Barabarani kuwa ajali nyingi zinasababishwa na madereva, wakiwemo wa Serikali ambao huvunja sheria kwa makusudi.

Hivyo, alitoa wito kwa trafiki kuwa wakali dhidi ya madereva wazembe, bila kujali kuwa ni wa magari yenye namba za usajili za Serikali.

Related Posts