“Leo nitakuwa live TikTok, kwahiyo uwahi”. “Eeeh…..nawahi space huko X (tweeter)”. Ni maneno ambayo husikika sana katika kona mbalimbali za mitaa ya majiji na miji nchini Tanzania, watu wakiwa bize na masuala ya mitandao.
Kumekuwa na wimbi kubwa la watu wanaotumia mitandao ya kijamii katika karne hii ya 21, na pengine si ajabu ni kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Wahenga walisema “ukiona zinduna, ambali iko nyuma”. Katika mazuri hapakosi kuwa na mabaya japo kwa uchache. Naam l, hata katika matumizi ya mitandao ya kijamii kuna pande mbili zinazokinzana.
Wakati watu wengine wakiamini mitandao ya kijamii inawasaidia kupata taarifa, kutafuta marafiki na wachumba, kujiingizia kipato na kutafuta fursa mbalimbali ikiwemo nafasi za masomo na ajira, wapo wanaoamini tofauti na hivyo. Ambapo wapo wanaoamini kuwa mitandao ya kijamii ni chanzo cha mmomonyoko wa maadili, kudolola kwa utamaduni, pia ni matumizi mabaya ya wakati.
Wanazuoni wakaenda mbali wakasema Mitandao ya kijamii endapo itatumika vizuri kwa kuzingatia maadili ya mtu na utu, basi itakuwa ni sehemu nzuri ya kujifunza na kujitafutia fursa.
“Kizazi cha leo ni kizazi cha kidijitali ambacho vitu vingi vya wakati wao vinapatikana mtandaoni”, alisema Ibrahim Mgaza, moja ya wanafunzi wa chuo kikuu cha uandishi wa habari na mawasiliano kwa umma UDSM. “Pia kizazi hiki, kinatumia mitandao ya kijamii kwa asilimia kubwa tofauti na shughuli yoyote ile”, aliongeza. Mitandao ya kijamii imeleta mabadiliko makubwa kwa kizazi cha leo, hasa katika mawasiliano, elimu, burudani, na ujumuishaji wa kijamii.
Vijana wanaweza kuwasiliana na marafiki na familia kwa urahisi, kupata habari na rasilimali za kielimu, na kufurahia burudani kupitia majukwaa kama WhatsApp, Facebook, Instagram, na TikTok. Aidha, mitandao hii imewawezesha kuunganishwa na watu wenye maslahi yanayofanana, kujenga jumuiya na mitandao ya kijamii, na pia kufanya biashara na kujipatia kipato.
Hata hivyo, mitandao ya kijamii pia imeleta changamoto kama vile shinikizo la kijamii, kulinganisha maisha na wengine, unyanyasaji mtandaoni, na athari kwa afya ya akili. Mabadiliko ya haraka katika mitindo, lugha, na tabia yameathiri maadili na utamaduni wa kizazi cha leo, hasa kutokana na ushawishi wa watu maarufu na “influencers”. Kwa ujumla, mitandao ya kijamii ina faida na changamoto ambazo zinaathiri maisha ya vijana kila siku ambapo wanatofautiana tu matumizi kwamba kila mmoja anakusudio lake.
#KonceptTvUpdates