Uwekezaji wa Sh3.24 trilioni kukabili uhaba wa mbolea nchini

Dar es Salaam. Kilio cha uhaba wa mbolea nchini huenda kikafikia ukomo, baada ya kusainiwa makubaliano ya ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha mbolea aina ya urea hapa nchini.

Makubaliano hayo  yamesainiwa kati ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) pamoja na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) na Kampuni ya Essa kutoka nchini Indonesia ya ujenzi wa kiwanda hicho.

Kulingana na Wizara ya Kilimo, wastani wa uzalishaji wa mbolea nchini kwa mwaka ni tani 114,223 na inayoingizwa kutoka nje ni tani 611,651 dhidi ya mahitaji ya tani 848, 884.

Katika mkataba uliosajiliwa leo Jumatano Julai 31, 2024, kiwanda hicho kitakuwa kikitumia gesi asilia na kitajengwa mkoani Mtwara. Kinatarajiwa kukamilika mwaka 2027, lakini uzalishaji wake utaanza miaka miwili baadaye.

Hatua hiyo imetajwa kuwa itaokoa mabilioni ya fedha zinazotumiwa na Serikali kama ruzuku kuagiza mbolea nje ya nchi, ambapo kwa takwimu hadi sasa asilimia kubwa ya mbolea inayotumika nchini inaagizwa kutoka nje.

Akizungumza baada ya utiaji saini huo uliofanyikia Jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema kiwanda hicho kutaifanya Tanzania kujitegemea kwa mbolea kwa asilimia 100.

“Wanawekeza jumla ya Dola bilioni 1.2 (Sh3.24 trilioni), nimeongea nao waharakishe na wamekubali, hivyo mradi huu unachagiza ajenda ya uchumi wa Tanzania,” amesema.

Profesa Mkumbo amesema asilimia 65 ya malighafi za viwandani zinategemewa kutoka katika shughuli za kilimo, hivyo hatua ya uzalishaji wa mbolea nchini itaongeza tija si tu katika kilimo, bali katika maendeleo ya viwanda.

“Kwenye ajira pia, vijana wetu watapata katika kiwanda hicho na shambani, kama Serikali tunaunga mkono kwa asilimia 100 uwekezaji huu hadi utakapoanza uzalishaji,” amebainisha.

Aidha, Profesa Kitila amesema uwekezaji huo ni matunda ya ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoifanya nchini Indonesia mapema mwaka 2024.

Kuhusu uwekezaji huo, Mkurugenzi Mtendaji TFRA, Joel Laurent amesema kiwanda hicho kitamsaidia mkulima wa Tanzania kupata mbolea kwa bei nafuu kwa ajili ya kuongeza uzalishaji.

Amebainisha kuwa matumizi ya mbolea yanaongezeka, kwani mwaka 2022/23 matumizi yalikuwa karibu tani laki tano na msimu 2023/24 yakapaa hadi zaidi ya tani laki nane na inatarajiwa kuwa yatafika tani milioni moja, hivyo kiwanda kimekuja wakati mwafaka.

“Pia, mpango wa ruzuku ya mbolea utaendelea hata katika mwaka ujao wa fedha 2025/2026, wakulima wote tunawaomba waendelee kujiandikisha, uzalishaji ukianza bei ya mbolea itakuwa nafuu na mkulima wetu ataimudu na gharama za Serikali kuhudumia mbolea itaondoka,” amesema.

Akitaja umuhimu wa urea, amesema pia ni chanzo cha uzalishaji wa mbolea nyingine. Amesema ni mbolea inayotumika moja kwa moja na vilevile kama malighafi ya mbolea nyingine.

Hata hivyo, akigusia umuhimu wa uwekezaji huo, Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Gilead Teri amesema ajira karibu laki nne zitazalishwa kupitia mradi huo tangu unapoanza katika ujenzi hadi uzalishaji.

Kaimu Mkurugenzi wa Mipango na Uwekezaji kutoka TPDC, Godbless Robiam amesema shirika hilo litawauzia Kampuni ya Essa gesi karibu nusu ya inayotumika nchini kwa sasa.

“Tutawauzia futi za ujazo milioni 70 kwa siku. Tumepata mteja mkubwa, lakini faida yake itaongeza uzalishaji wa gesi. Kingine TPDC itashiriki katika mnyororo mzima,” amesema.

Mwakilishi mkazi wa kampuni ya Essa, Abdallah Kitete, amesema uzalishaji wao unategemea gesi na kwa makubaliano waliyoyafanya kuna uwezekano wa kupewa gesi mwakani wakaanza kujenga kiwanda hicho.

“Tutazalisha tani milioni moja kwa mwaka, lakini kwa uhitaji wa nchi kwa sasa kunahitajika tani laki nane na nusu za mbolea, hivyo tutauza katika nchi za Jumuiya ya maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

“Tutakuwa na awamu tatu. Tutaweka Dola bilioni 1.2, ya kwanza tutaanza baada ya kukamilika kwa kiwanda na kila awamu tutaongeza uzalishaji kila tutakapoongezewa gesi,” amesema.

Amesema uwekezaji wao ni miaka 20, kila awamu na awamu ya kwanza na pili ni miaka 40, kisha wataongeza awamu ya tatu kufikia miaka 60.

“Sisi tunawekeza moja kwa moja na tutatoa ajira kwanza, ujenzi wa kiwanda na baada ya kuanza uzalishaji kwa Watanzania tutapunguza matumizi ya dola katika uagizaji wa mbolea kwa kuwa itazalishwa ndani,” amesema na kuongeza;

“Tukianza kuzalisha maana yake hata bidhaa kama mafuta ya kula yataanza kuzalishwa hapahapa nchini, hii ni hatua kubwa na kilimo kitakuwa biashara kwa maana uhakika utakuwa mkubwa.”

Kuhusu uwekezaji huo, mchambuzi wa uchumi, Dk Mwinuka Lutengano amesema Tanzania ilikuwa na mahitaji mkubwa ya mbolea na kupunguza utegemezi wa nje.

Amesema kuzalisha mbolea aina ya urea nchini ni hatua kubwa iliyokuwa ikisubiriwa hasa na wakulima, sasa kinachosubiriwa ni kuona iwapo uwekezaji huo utaleta unafuu wa bidhaa hiyo na kupunguza gharama ya uzalishaji wa mazao kwa wakulima.

“Haya yote yatawezekana hasa kama mbolea hiyo itazalishwa kwa teknolojia nzuri, ili bei iwe na unafuu kuliko ingeagizwa kutoka nje. Pia tozo na kodi ndogo za ndani ziwe kama mbadala wa ruzuku. Tija kwenye kilimo itakuwa kubwa,” amesema mchumi huyo.

Mchambuzi mwingine, Oscar Mkude amesema uwekezaji huo ni hatua muhimu kwa sekta ya kilimo, ukizingatia kilimo kinashika nafasi ya pili kwenye mchango wa uchumi wa Tanzania baada ya sekta ya huduma.

“Sekta ya kilimo ndio mwajiri mkuu na kilimo ndio sekta yenye tija ndogo zaidi (lowest productivity). Hii inafanya jitihada za kumletea Mtanzania maendeleo ziwe zinazoleta mabadiliko kwenye sekta ya kilimo,” amesema.

Hata hivyo, amesema hii si mara ya kwanza kusikia nia kama hiyo ya kuwekeza, kwani tumeshawahi kuwa na nia ya kuwa na kiwanda cha mbolea kwa kutumia malighafi ya gesi, lakini, ndoto/nia hiyo hakijatimia hadi sasa.

“Ni muhimu zaidi kujizatiti katika hatua ya kuitekeleza nia. Bahati mbaya, huwa tunaonyesha kufurahi zaidi au hata kujipongeza kwa kusaini mikataba ya makubaliano, lakini sote tunafahamu inahitaji jitihada zaidi kutekeleza miradi kama hii na hapo kuna changamoto labda ndio udhaifu wetu ulipo,” amesema Mkude.

Related Posts