Usafirishaji wa dharura watajwa kupunguzwa vifo wajawazito, watoto wachanga

Arusha. Mkoa wa Arusha umefanikiwa kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga kutoka vifo vitokanavyo na uzazi 67 mwaka 2022/23 hadi vifo 48 mwaka 2023/24. Hii ni sawa na upungufu wa asilimia 28.3, ikiwa ni mwaka mmoja tu tangu mkoa huo uanze  kutekeleza mpango wa usafirishaji wa dharura wa wajawazito na watoto wachanga, ujulikanao kama m-mama.

Akizungumza jijini Arusha leo Jumatano, Julai 31, 2024, Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Edna Ntulle amesema tangu mpango huo uzinduliwe mkoani hapa, umeanza kuonesha matokeo chanya katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.

Dk Ntulle amefafanua kuwa mfumo huo ambao ulianzishwa Desemba 19, 2020 na kuanza kutekelezwa rasmi Machi 2023, umechangia kupunguza vifo vya wajawazito na watoto kwa vifo 19, sawa na asilimia 28.3.

“Mkoa umeendelea kupunguza vifo kupitia mikakati mbalimbali ikiwemo huu, takwimu zinaonesha mwaka 2022/23 kulikuwa na vifo 67, lakini idadi hiyo imepungua hadi kufikia vifo 48 mwaka 2023/24,” amesema.

Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Missaile Musa amezitaka halmashauri za mkoa huo kutenga fedha kwenye bajeti zao za kila mwaka kwa ajili ya kuchangia mfuko wa Afya wa Taifa, ili kuwezesha utekelezaji wa mpango huo. Amesema mpango huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga na kusisitiza baadhi ya halmashauri ambazo hazijawalipa madereva wanaofanya kazi hiyo, zihakikishe malipo hayo yanafanyika mara moja.

“Ni agizo la Serikali kwamba kila halmashauri itenge fedha kwa ajili ya kuendesha programu ya m-mama na kuhakikisha madereva wanaosafirisha wagonjwa wanalipwa kwa wakati, hakuna sababu ya kulimbikiza madeni yao,” amesema.

Kwa upande wake, Muuguzi Mkuu na Mratibu wa m-mama Mkoa wa Arusha, Getrude Anderson amesema kupitia mfumo huo wa usafiri na rufaa ya dharura kwa wajawazito na watoto wachanga, wataendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya namna ya kunufaika na huduma hiyo.

Anderson ameongeza kuwa kikao kazi kilichofanyika kililenga kutambua changamoto na kuweka mikakati ya utatuzi, ikiwemo kufuatilia vifo vitokanavyo na uzazi, kuwajengea uwezo watoa huduma na kuimarisha matumizi ya kanzidata.

Mmoja wa wananchi wa Mtaa wa Suye, Kata ya Olorien jijini Arusha, Anastazia Kivuyo amesisitiza umuhimu wa Serikali kuendelea kutangaza mpango huo kwa jamii, hususan katika maeneo ya pembezoni ambako wananchi hulazimika kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma za afya.

“Kiukweli mimi binafsi nimeanza kuisikia siku za karibuni, ninaamini elimu inapaswa kutolewa zaidi kwa jamii ili wananchi waweze kuifahamu na itasaidia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi hasa kwa maeneo ya vijijini,” amesema.

Related Posts