Watanzania wapania kuiteka gofu Mombasa

WACHEZAJI watano wa gofu kutoka Tanzania, wanatarajia kuondoka nchini mwishoni mwa juma kwenda kushiriki michuano ya wanawake iliyoandaliwa na Chama cha Gofu ya Wanawake Kenya (Kenya Ladies Golf Union), kuanzia Jumatatu, Agosti 5.

Mashindano hayo yanayoshirikisha wacheza gofu wa kike kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki wakiwakilisha Kenya, Uganda na Tanzania na yatafanyika katika viwanja vitano tofauti katika miji ya mwambao wa kenya ya Mombasa, Vipingo na Malindi ili kupata mshindi wa jumla.

Wacheza kutoka Tanzania ambao wamepania kuiteka tena Mombasa kwenye mashindano hayo kama ilivyokuwa mwaka jana ni Vicky Elias wa Klabu ya TPDF Lugalo, Yasmin Challi na Shaz Myombe kutoka Dar Gymkhana, Neema Olomi, Arusha Gymkhana na Loveness Mungure wa Kili Gollf pia ya Arusha.

“Sihitaji kufanya mazoezi sana katika viwanja hivyo vitano vya nje ya nchi, kwani nafahamu kila pembe yake, kwa hiyo havitanipa tabu hata kidogo kuvimudu na ushindani utakaojitokeza,” alisema Vicky, mmoja wa wachezaji tegemeo.

Katika mashindano ya mwaka jana, Tanzania ilifanya vizuri baada ya kushinda nafasi mbili kati ya tatu za juu katika mchezo wa mashimo 18 ya ufunguzi katika viwanja vya Mombasa Leisure lodge.

Olomi alimaliza wa pili baada ya kurudisha mikwaju 79, licha ya kufungana kwa idadi hiyo hiyo ya mikwaju na Vicky, lakini sheria ya kuhesabu nani kafanya vizuri mwishoni(countback) ilimpa Vicky nafasi ya tatu.

Mungure, ambaye mwaka jana alishinda mashindano ya wanawake ya Zambia, pia alifanya vizuri katika michuano hii ya Pwani ya Kenya mwaka jana baada ya kumaliza wa tatu katika mfumo wa kuhesabu neti.

“Tulifanya vizuri mwaka jana na tunategemea kufanya vizuri zaidi katika mashindano ya mwaka huu,” alisema Olomi baada ya mazoezi ya kina katika viwanja vya Gymkhana, Arusha.

Baada ya kumaliza raundi ya kwanza katika viwanja vya Leasure Club, Watanzania watakuwa na kibarua kingine Jumanne na watashiriki katika mchuano wa mashimo 36 katika viwanja vya Nyali kabla ya kwenda Malindi Golf Club na watacheza mashimo mengine 18.

Mtihani wao wa mwisho utakuwa katika viwanja vya Vipingo Ridge watakapomalizia raundi ya tano.

Related Posts