Dar es Salaam. Shahidi wa pili wa utetezi katika kesi ya mkopo tata baina ya Kampuni ya Kahama Oil Mills Limited na wenzake dhidi ya Benki za Equity Tanzania Limited (EBT) na Equity Kenya Limited (EBK) amewabainisha wakopaji halisi wanaodaiwa katika kesi hiyo.
Pia shahidi huyo, Timothy Mwatha ambaye ni Meneja Mkuu wa Mikopo wa Kampuni wa EBK ameelezea mchakato wa ufanikishaji utolewaji wa mkopo huo na namna ulivyohamishwa kutoka kwa wakopesha kwenda kwa wakopaji.
Shahidi huyo ametoa maelezo hayo wakati akiongozwa na wakili wa utetezi, Zaharani Sinare kufafanua baadhi ya maelezo katika maelezo ya ushahidi wake aliokwishauwasilisha mahakamani kwa njia ya maandishi na wakati akihojiwa maswali ya dodoso na wakili wa wadai katika kesi hiyo, Frank Mwalongo.
Sambamba na ufafanuzi huo wa maelezo ya ushahidi wake huo wa maandishi alioutoa jana Jumatatu Julai 30, 2024 kuanzia mchana mpaka saa moja usiku, vilevile shahidi huyo amewasilisha nyaraka mbalimbali zilizopokewa na mahakama kuwa vielelezo vya ushahidi.
Kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Profesa Agatho Ubena, Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, Dar es Salaam imefunguliwa na Kampuni za Kahama Oil Mills Limited na Kahama Import & Export Commercial Agency Limited, zinazodaiwa kukopeshwa fedha hizo na benki hizo.
Wadai wengine katika kesi hiyo namba 78 ya mwaka 2023 ni wadhamini wa mkopo unaobishwaniwa; Kom Group of Companies Limited, Shinyanga Royal Pharmacy (2015) Limited, Royal Supermarket (2008) Limited na Mhoja Nkwabi Kabalo, mkurugenzi wa kampuni hizo.
Kesi hiyo ni miongoni mwa kesi kadhaa zilizofunguliwa dhidi ya benki hizo na kampuni mbalimbali zinazodaiwa kukopeshwa na benki hizo mabilioni ya fedha kisha zikazifungulia kesi benki hizo zikipinga kudaiwa kwa madai kwamba hazikukopeshwa na benki hizo au zimeshalipa mkopo.
Kampuni hizo zilifungua kesi hiyo baada ya kuandikiwa barua na benki hizo zikiwataka kulipa Dola za Marekani 46,658,395.81 (zaidi ya Dola za Marekani 46.6 milioni sawa na zaidi ya Sh122.54 bilioni).
Kwa mujibu wa kumbukumbu za mahakama, kampuni hizo zinadai hazijawahi kupokea mkopo wa Dola 32 milioni kutoka kwa wadaiwa katika kesi hiyo, benki hizo huku wakidai benki hizo zilitoa mkopo huo kwa Kampuni ya Kom Group of Companies ya Nairobi Kenya.
Badala yake zinadai zenyewe zilipokea mkopo wa Dola 30 milioni kutoka kwa Kom Group of Companies Limited ya Nairobi Kenya ambayo haihusiki katika kesi hiyo na si kwa wadaiwa yaani benki hizo na kwamba tayari zilishaanza kulipa sehemu ya mkopo huo.
Benki hizo nazo zilifungua madai kinzani dhidi ya kampuni hizo zikisisitiza kuzikopesha mkopo ambao hazikuurejesha, huku zilipinga na kuzitaka zithibitishe kuwepo kwa kampuni inayoitwa Kom Group of Companies Limited ya Nairobi Kenya ambayo kampuni hizo zinadai ndio ilikopeshwa na benki hizo.
Kwa mujibu wa benki hizo kwa sasa deni hilo limefikia Dola za Marekani 47,228592.53. (zaidi ya Sh123 bilioni) kiasi kinachojumuisha deni la msingi la mkopo wa Dola 32 milioni pamoja, riba na faini.
Katika ushahidi wake, Mwatha amesema mkopaji katika kesi hiyo ni Kahama Oil Mills Limited na Kahama Import & Export Commercial Agency Limited na si Kom Group of Companies ya Nairobi kama ambavyo wadai katika kesi hiyo (wakopaji) wanavyodai.
Mwatha amefafanua Kom Group of Companies Limited, (ambayo inatambuliwa kwa anuani ya EBK, Nairobi Kenya) ni jina la akaunti ya ndani ya mkopo ambayo ilifunguliwa na EBK kwa ajili ya kufanikisha utolewaji wa mkopo huo.
Kwa mujibu wa upande wa utetezi na kama hati ya madai kinzani unavyoeleza, kampuni hizo hazikuwa na akaunti ya kawaidai ndani ya EBK, kwa kuwa ni benki ya nje.
Hivyo ili kufanikisha utolewaji, uhamishaji na urejeshwaji wa mkopo huo, EBK ilifungua akaunti mbili kwa ajili mkopo huo.
Akaunti hizo ni hiyo ya mkopo wa ndani yenye jina la Kom Group of Companies Limited kwa kutumia anuani yake (EBK) ya Nairobi Kenya ili kufanikisha utolewaji wa mkopo huo.
Nyingine ni akaunti ya Escrow, kwa jina la Kahama Oil Mills Limited -Escrow account, pia kwa anuani ya EBK, ili kuwezesha uhamishaji wa mkopo huo kwenda katika akaunti ya mdaiwa wa kwanza, Kahama Oil Mills.
Hivyo kwa mujibu wa Mwatha akaunti hizo zilitumika kwa ajili ya kufanikisha mtiririko wa mkopo wa Dola za Marekani 26,592, 232.00, uliotolewa na EBK, mpaka kufikia mkopaji kwenda kwenye akaunti yake.
Sambamba na maelezo yake pia amewasilisha nyaraka mbalimbali zinazohusiana na mchakato na utolewaji wa mkopo huo, ambazo zimepokewa na Mahakama na kuwa vielelezo vya ushahidi katika kesi hiyo.
Nyaraka (vielelezo) hivyo ni pamoja na taarifa za fedha za akaunti za benki zilizotumika katika utolewaji wa mkopo huo, ambazo zinakusudiwa kuonesha mtiririko wa miamala ya fedha hizo, kutoka kwa wakopeshaji kwenda kwa wakopaji.
Wakati akihojiwa maswali ya dodoso na Wakili wa wadai katika kesi hiyo, Mwalongo, amefafanua mkopo huo kutoka EBK ulikwenda katika akaunti ya ndani ya EBK yenye jina Kom Group of Companies Limited, kisha kwenda katika akaunti ya ndani Escrow ya EBK yenye jina la Kahama Oil Mills Limited.
Amekiri mkopo huo kwenda kwa wadai ulitoka akaunti ya Escrow na kwamba akaunti hizo mbili zote lengo lake ni kufanikisha utoaji na ulipaji wa mkopo husika.
Amehitimisha ushahidi wake baada ya Wakili Sinare, kuileza Mahakama hana maswali ya ufafanuzi kutokana na majibu yake ya maswali ya dodoso aliyoulizwa na Wakili Mwalongo.
Baada ya shahidi huyo kuhitimisha ushahidi wake, Wakili Sinare ameieleza Mahakama hiyo kuwa bado wanaye shahidi mwingine ambaye watamuita kuendelea kutoa ushahidi.
Jaji Ubena ameahirisha kesi hiyo hadi Agosti 21, 2024 itakapoendelea kwa ushahidi wa upande wa utetezi.