Dar es Salaam. Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart) imesitisha safari zake kupitia barabara za Morogoro na Kawawa jijini Dar es Salaami kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini na kusababisha mafuriko eneo la Jangwani na Mkwajuni.
Hii si mara ya kwanza kuchukuliwa kwa hatua hiyo, mwanzoni mwa wiki hii Dart ilisitisha huduma kati ya Kimara hadi Kivukoni na Gerezani baada ya eneo la Jangwani kujaa maji.
Taarifa ya leo Ijumaa Aprili 26, 2024 iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano Dart imeeleza mabasi kwa njia za Kimara hadi Kivukoni, Gerezani na Morocco yanaishia Magomeni Mapipa.
“Huduma ya usafiri wa Mabasi ya Dart inaendelea kutolewa eneo la katikati ya Jiji kwa njia ya Muhimbili na Gerezani.
Pia, huduma za mabasi katika mfumo wa Dart zinaendelea kama kawaida katika njia za Kimara hadi Mbezi, Kimara hadi Kibaha na Kimara hadi Mloganzila,” imeandikwa kwenye taarifa hiyo.
Taarifa ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) iliyotolewa jana Alhamisi imebainisha mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika maeneo mengi nchini zinatarajiwa kukoma Aprili 28, 2024.
Usiku wa kuamkia leo Ijumaa, maeneo mengi nchini ikiwamo Dar es Salaam yamekuwa na mvua kubwa na kusababisha maeneo mbalimbali kujaa maji.
Katika ufafanuzi wake wakati akizungumza na Mwananchi Digital, Mkurugenzi Mtendaji wa Dart, Dk Athaman Kihamia amesema: “Wito wangu kwa wananchi wawe na subira kwa sababu eneo hilo la Jangwani lenye shida hivyo Serikali imeshalitolea fedha za kutosha kupitia mradi wa DMDP, kwa hiyo patajengwa hapo na daraja la juu litajengwa itakuwa suluhuisho.”
Dk Kimamia katika maelezo yake amesema kwa sasa hivi mvua ni kitu ambacho kipo nje ya uwezo wa binadamu, wananchi wanapaswa kuwa makini hata wenye magari madogo wasipite eneo hilo kwa usalama wa maisha na mali zao.
“Licha ya kuwa na foleni, wananchi waache kutumia njia za mwendokasi kupitia kwani ni maalumu kwa mabasi na si kwa ajili ya matumizi mengine au watembea kwa miguu au magari mengine,” amesema.
Endelea kufuatulia Mwananchi kwa habari na taarifa mbalimbali.