Hali mbaya kiuchumi kwa mawakili yamkera Sungusia

Dodoma. Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Harold Sungusia amesema anasikitishwa na baadhi ya mawakili kuacha taaluma hiyo na kujiingiza kwenye biashara ndogondogo kujikimu kimaisha.

Sungusia ameyasema hayo Julai 31, 2024 wakati mkutano mkuu wa Chama cha Wakili Welfare Mkoba, kinachojumuisha mawakili wa kujitegemea na Serikali.

Amesema wataendelea kuhamasishana na kufanya kazi kwa pamoja kukiboresha chama hicho ili wakili aweze kufanya kazi zake kwa umahiri, katika mazingira bora na kujisikia yuko vyema.

“Inasikitisha unapokuta wakili anauza ubuyu huko mtaani, anauza maandaazi, naamini hiyo financial prosperity (ustawi wa kiuchumi) itamsaidia kila wakili ajisikie raha,” amesema.

Kwa upande wake, Kamishna wa Wizara ya Fedha, Dk Charles Mwamwaja aliyekuwa mgeni rasmi katika mkutano huo amesema bado watumiaji wa huduma za kifedha ni wachache.

 “Kwa mujibu wa utafiti uliofanyika mwaka jana unaonyesha kuwa ni asilimia 21 tu ya nguvu kazi ya Taifa ndio iliyofikiwa na huduma ndogo za fedha,” amesema.

Amesema huduma za kifedha kama Vikoba iliyoanzishwa na mawakili hao ni jambo jema, hivyo ni vizuri Watanzania wote kwa wingi waende katika njia hiyo.

Amesema Serikali imefanya mambo mengi mazuri kuhakikisha sekta hiyo inasimamiwa na kufanyiwa kazi ikiwemo kutunga sera ya huduma ndogo za fedha, Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha na kanuni zake.

 “Kwa hiyo niwasihi hizi nyenzo ni muhimu, tupate muda wa kusoma sera inasemaje, sheria inasemaje na kuwalinda watumiaji wa huduma za fedha,” amesema.

Amesema watoa huduma za fedha wanatakiwa kuwaelimisha watumiaji wa huduma hizo ili kujua haki zao ni zipi.

Meneja wa Kanda wa Biashara Ndogo na Kati wa Benki ya ABSA, Walter Migambile ambao ni wadhamini wa mkutano huo, amesema wataendelea kushirikiana na jamii kama walivyofanya kwa mawakili hao.

Wakili wa Kujitegemea, Boniface Mwabukusi amesema kuanzishwa kwa huduma hiyo ya Vicoba ni jambo bora, la kiungwana na la muhimu katika kuwawezesha mikopo yenye riba nafuu.

“Ni muhimu kujiunga, kushirikiana, kuwezeshana kupata fedha kupitia taasisi hii. Mnaweza kupata mikopo mikubwa kwa sababu mnafahamiana, mnajua kusimamiana na kudhibitiana,” amesema.

Mkurugenzi wa Wakili Welfare Mkoba, Laetitian Tagazwa amesema uamuzi wa kuanzisha kikoba hicho, umetokana na madhila na hali ngumu ya kiuchumi wanayopitia mawakili ikiwemo kukutana na mikopo yenye riba kubwa kutoka katika taasisi na mabenki.

Amesema hivi sasa wana wanachama 305 ambao ni mawakili wa Serikali na wa kujitegemea na wana mtaji wa Sh220 milioni.

Related Posts