TUME YA RAIS YA KUTATHMINI NA KUSHAURI MASUALA YA KODI YAUNDWA – MWANAHARAKATI MZALENDO

Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameunda Tume ya Rais ya Kutathmini na Kushauri kuhusu Masuala ya Kodi na kumteua Balozi Ombeni Yohana Sefue, Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu, kuwa Mwenyekiti wa Tume hiyo. Uteuzi huu unafuatia tangazo lake la tarehe 29 Julai 2024 wakati wa Mkutano wa 15 wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), ambapo alitangaza uamuzi wa Serikali kuunda kamati ya kutathmini na kushauri kuhusu masuala ya kodi nchini.

Tume hiyo pia inajumuisha wajumbe mashuhuri kutoka sekta mbalimbali. Wajumbe walioteuliwa ni pamoja na Prof. Florens Luoga, aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Profesa Mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na Prof. Mussa Juma Assad, aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Profesa Mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Wengine ni Leonard Mususa, aliyekuwa Afisa Mtendaji Mkuu wa PricewaterhouseCoopers (PwC) Tanzania, CPA. Aboubakar Mohamed Aboubakar, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU), na Balozi Mwanaidi Sinare Maajar, Mshauri wa Masuala ya Sheria.

Pia, tume hiyo inajumuisha David Tarimo, Mtaalam na Mshauri wa Masuala ya Kodi na aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Ushauri wa Kodi, PwC, Balozi Maimuna Kibenga Tarishi, Katibu Mkuu Mstaafu, na Rished Bade, Kamishna wa Fedha za Nje, Wizara ya Fedha na aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Tume hii imepewa jukumu la kutathmini hali ya kodi nchini na kutoa ushauri kwa Serikali ili kuboresha mfumo wa kodi na kuhakikisha uwajibikaji na ufanisi katika ukusanyaji wa mapato. Rais Samia alieleza matumaini yake kuwa tume hii italeta mabadiliko chanya katika mfumo wa kodi na kusaidia kukuza uchumi wa nchi.

#KonceptTvUpdates

Related Posts