Dar es Salaam. Historia inaandikwa leo . Hivyo ndivyo inavyoelezwa na kila aliyehudhuria uzinduzi rasmi safari za treni ya umeme (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma.
Mapema Julai 2024, treni ya kisasa ilianza kufanya safari za Dar es Salaam na Morogoro na baadaye zikaongezwa za Dar es Salaam na Dodoma.
Kuanza kwa safari hizo, ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan alilolitoa Desemba 31, 2023, wakati akitoa salamu za mwaka mpya 2024, akilitaka Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuhakikisha danadana zinakwisha na safari za treni ya SGR zinaanza ifikapo Julai, 2024.
Leo Alhamisi Agosti mosi, 2024 Rais Samia anazindua safari hizo na kusafiri na treni hiyo, akiwa ameambatana na viongozi kadhaa wa Serikali na vyama vya siasa.
Mapema asubuhi viongozi mbalimbali, wakiwemo mawaziri, wabunge na viongozi wa CCM waliwasili Stesheni ya Dar es Salaam kushuhudia uzinduzi rasmi wa safari hizo zilizoanza Julai 25, mwaka huu.
Mbali na viongozi hao wa chama tawala, walikuwepo pia viongozi wa vyama vya upinzani akiwemo Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba ma Mwenyekiti wa Chaumma, Hashim Rungwe.
Akizungumza stesheni hapo, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla amesema kuanza kwa safari hizo za reli ya SGR kunaifanya Tanzania kuandika historia ya kuwa na treni ya kisasa, ikilinganishwa na nchi nyingine Afrika ambazo tayari zina usafiri huo.
Makalla amesema nchi mbalimbali zimekuja kujifunza kwa kilichofanyika Tanzania, hivyo Watanzania wanapaswa kujivunia kazi hiyo na kuhakikisha wanaitunza na kuilinda miundombinu.
“Tuna kila sababu ya kujipongeza kwa kazi kubwa iliyofanyika, tunaandika historia sasa ili iendelee kudumu, ni muhimu tukawa wazalendo na kuitunza miundombinu hii iendelee kuturahisishia usafiri kama tunavyoona sasa ndani ya muda mfupi unafika Dodoma.
“Furaha yetu si tu kusafiri ndani ya muda mfupi, bali treni hii inakwenda kuchangamsha uchumi, biashara zitafanyika kwa haraka zaidi watu wataweza kwenda na kurudi Dodoma na shughuli nyingine zikaendelea,” amesema Makalla.
Mbali na hilo, Makalla amesema kukamilika kwa mradi huo kunadhihirisha kazi inayofanywa na Serikali ikitoa majibu kwa wale wanaopiga kelele za kuongezeka kwa deni la Taifa.
“Yaani hapa ndiyo inadhihirika kwamba mikopo inayokopwa inatumika kwenye miradi ya maendeleo ambayo inaleta matokeo chanya.
“Zile kelele za kukopa na kuongezeka deni la Taifa, nafikiri Watanzania watakuwa wamejionea fedha zinazokopwa zinatumikaje kwa ajili ya maendeleo yao,” amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amewataka wakazi wa jiji hilo, hasa katika maeneo ambayo miundombinu ya reli inapita kuhakikisha wanakuwa sehemu ya ulinzi ili kuepusha uharibifu.
Chalamila pia amewataka watoaji huduma wengine za usafiri kutofikiria kufanya hujuma dhidi ya treni hiyo kwa kuhofia biashara zao kudorora.
“Uwepo wa treni hii haimaanishi kwamba vyombo vingine vya usafiri vitakosa abiria au vitazuiwa kutoa huduma, biashara yao itaendelea kama kawaida, hivyo nawasihi wasije wakafanya hujuma,” amesema Chalamila.