VIDEO: Mapito wanawake waliotelekezwa na waume zao Bwawa la Mtera

Dodoma. Wazazi wana jukumu la malezi ya watoto, lakini hali imekuwa tofauti kwa baadhi ya familia ziishio pembezoni mwa Bwawa la Mtera wanaolelewa na mzazi mmoja pekee.

Mwananchi Digital imebaini kwa kiasi kikubwa familia katika maeneo hayo zinaongozwa na wanawake baada ya wanaume kuzitelekeza.

Hali hii imeonekana kwenye vijiji vya Wilaya ya Iringa mkoani Iringa na wilaya za Mpwapwa na Chamwino za Mkoa wa Dodoma, ambavyo kwa miaka kadhaa vinategemea shughuli za uvuvi katika Bwawa la Mtera kuendesha familia zao.


Wavuvi wazikimbia familia zao wawaachia wanawake mzigo wa kulea watoto Mtera kisa upungufu wa samaki

Changamoto ya wanaume kutelekeza familia inatokana na kupungua samaki bwawani kwa zaidi ya miaka mitano sasa, hivyo kusababisha wakose vipato.

Veronica Haule, mkazi wa Kitongoji cha Kenya, wilayani Iringa ni miongoni mwa wanawake waliotelekezwa na waume zao baada ya samaki kupungua katika Bwawa la Mtera.

Mwandishi wa gazeti la Mwananchi, Sharon Sauwa akifanya mahojiano na Veronica Haule ambaye ni Mkazi wa Kitongoji cha Kenya Wilaya ya Iringa mkoani Iringa. Picha na Merciful Munuo

“Tangu mume wangu aliponiaga miaka miwili iliyopita kwamba anaenda Rukwa kutafuta kipato kutokana na hali ngumu ya uchumi hapa kijiji, hajawahi kurejea wala sijawahi kuwasiliana naye,” anasema Veronica, ambaye wakati wa mazungumzo na Mwananchi Digital alikuwa akichemsha mahindi kwa ajili ya chakula cha mchana kwenye jiko la kuni alilolitengeneza chini ya mti.

Anasema mlo wa familia yake yenye watoto sita unategemea kazi ya vibarua anayofanya ikiwamo palizi kwenye mashamba ya wanakijiji na kuuza kuni kijijini hapo.

“Naomba Serikali inisaidie mtaji niweze kufanya biashara, kama hivi unavyowaona hapa (watoto) wengine nimeshindwa kuwapeleka shule kwa sababu sina hela ya kununua mahitaji yao,” anasema.

Veronica anawazungumzia watoto wake wawili wanaohitaji kupelekwa shule, mmoja darasa la kwanza na mwingine shule ya awali.

Kutokana na kukosa fedha za kuwanunulia mahitaji, anasema alienda kwa diwani wa kata yake aliyemruhusu kuwapeleka shule pasipo kuwa na sare.

Humphery Njohoka, mvuvi katika bwawa hilo anasema kutokana na kupungua samaki, wapo wenzao waliohama na kuziacha familia zikiteseka kwa kukosa huduma.

“Hata mimi niliondoka kwa miaka miwili na kuiacha familia yangu, nilienda Rukwa ambako hali kidogo ilikuwa nzuri. Watoto niliwaacha wakiwa na hali mbaya. Kidogo nilichopata nilirejea kulea familia,” anasema.

Mwenyekiti wa kitongoji hicho, Mariam Njowoka anasema upungufu wa samaki umefanya wanaume kuzikimbia familia zao na kuwaacha wanawake wakihangaika kuwatunza watoto.

“Kesi nyingi nimezipata kuhusu wanaume kukimbia familia zao, nimezifikisha ofisi ya kijiji, tukawatafuta lakini hatujawapata,” anasema.

Njooka anasema katika kipindi cha kati ya mwaka 2023 na mwaka huu, amepata kesi tano za wanaume kukimbia familia zao kutokana na hali ngumu ya uchumi.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mtera, wilayani Mpwapwa, Mkoa wa Dodoma, Simon Lukui anasema walioenda kuvua maeneo mengine waliondoka bila familia kwa sababu hawakujua hali ambayo wangeikuta walikoenda.

Anasema walikoenda kufanya uvuvi hawana makazi ya kudumu, hivyo wanaishi kwenye katika makazi ya muda waliyotengeneza kwa kutumia maturubai.

“Changamoto ziko nyingi, kuna wakati wanawake wanakuja ofisini wakilalamika watoto wameshindwa kwenda shule kwa sababu hawana vifaa. Kwa hiyo, sisi tunachukua jukumu la kuwatafuta waliko na waume zao na kuwaeleza wake zao wamekuja kuripoti hawana mawasiliano,” anasema Lukui.

Lukui anasema baadhi ya wanaume wakishaelimishwa na kuelezwa kuwa watachukuliwa hatua iwapo hawatunzi familia, hujirekebisha.

Hata hivyo, anasema wapo ambao huzima simu na kuhama eneo walilopo hivyo kutopatikana.

Lukui anasema kwa mwaka hupokea wastani wa kesi tano za wanawake wanaofika kudai talaka.

Anasema wamekuwa wakiwasihi na kuwaomba wawape muda wa kuwatafuta wenza wao ili watekeleze majukumu yao ya malezi kwa familia.

Licha ya mazingira ya kiuchumi kuwa magumu, Lukui anasema hakuna matukio ya wanafunzi wengi kutohudhuria masomo.

“Shule ya msingi ina watoto kama 1,200, mwalimu anakuletea taarifa watoto 40 ni wazembe wa kufika shuleni, ni wachache sana. Hawa wanatoka kwenye familia zinazojishughulisha na shughuli nyingine za kiuchumi,” anasema.

Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Iringa, Erick Bange anasema watoto hawahudhurii vizuri masomo kwa sababu mama zao wanashindwa kugharamia mahitaji yao ya shule, ikiwemo sare na chakula.

Anasema wanaendelea kuhamasisha jamii kupitia mikutano ya hadhara na vikundi vya ujasiriamali kuhusu namna wanavyoweza kupata vipato vya kujikimu na kuwalea watoto.

“Kuna vikundi vinavyoanzishwa vya mabaraza ya watoto ambavyo vinalenga kuwatambua walio katika mazingira magumu, kujua wapi walipo na ikiwezekana kuwatafutia michango na kutambua mahitaji yao ili kuwasaidia,” anasema.

Anasema pia kuna mashirika yasiyo ya kiserikali yanayoenda maeneo ya wavuvi kutambua changamoto na kuweka mikakati ya kuzitatua.

Bange anataja changamoto zilizopo kuwa baadhi ya wanawake walioachwa na wenza wao, wengi wakiwa na umri wa miaka 15 hadi 35, wamekuwa na uhusiano usio rasmi na hauna staha.

Anasema wamekuwa na uhusiano huo na madereva wa malori ili kujikimu wao na familia zao.

Kutokana na changamoto hiyo, Bange anasema wamekuwa wakitoa elimu kwa wanawake hao jinsi ya kutumia njia nyingine kujikimu.

Bange anasema jitihada nyingine zinazofanyika ni kuwapa mikopo kutoka halmashauri inayotolewa kwa wanawake, vijana na wenye ulemavu.

Pia, anasema vimeanzishwa vikundi vya malezi na makuzi ya watoto vikilenga kuwatambua na kusikiliza changamoto zinazowakabili.

Changamoto nyingine anasema ni watoto kuolewa katika umri mdogo baada ya kumaliza darasa la saba, hivyo kuwakosesha fursa ya kuendelea na masomo.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Robin Gama anawashauri kutafuta fursa nyingine za kujiingizia kipato badala ya kutelekeza familia.

“Watoto wanapoenda shule kupata elimu tunailea jamii itakayokuja kuwa na nguvu na baadaye katika umri wa uzee watataka vijana wawatunze vizuri,” anasema.

Habari hii imeandaliwa kwa kushirikiana na Bill & Mellinda Gates

Related Posts