Kamera za uchunguzi takribani 6500 kupunguza uharifu na kuimarisha ulinzi na usalama nchini

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Daniel Sillo amesema Serikali iko mbioni kufunga mitambo ya Kamera za uchunguzi takribani 6500 kwa kuanzia na majiji makuu manne ili kupunguza uharifu na kuimarisha ulinzi na usalama kwa Wananchi.

Kauli hiyo imetolewa Julai 31, 2024 na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Nchini, Mhe. Daniel Sillo (Mb) wakati akiwa kwenye ziara ya kikazi Mkoani Kagera alipokutana na Taasisi ambazo ziko chini ya Wizara hiyo ikiwemo Jeshi la Polisi, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Jeshi la Magereza, Idara ya Uhamiaji pamoja na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa NIDA na kufanya nao Mkutano sambamba na kusikiliza changamoto zinazowakabili.

Akizungumza katika Mkutano huo Naibu Waziri Sillo, amesema kuwa Serikali ipo mbioni kufunga Kamera zaidi ya 6500 ambazo lengo likiwa ni kusaidia kufichua watu wanaojihusisha na vitendo vya uharifu pamoja na kuimarisha suala la ulinzi na usalama kwa Wananchi na mali zao hapa nchini.

Amesema kuwa, Kamera hizo zitafungwa katika maeneo ya mikusanyiko ya watu wengi kama masoko, viwandani na kwenye makampuni ikiwemo kwenye majiji makuu manne nchini ambayo ni Arusha, Mwanza, Dodoma pamoja na Jijini la Dar es Salaam.

”Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassani kwa kipindi cha uongozi wake tunajivunia mengi kwani ameimarisha vyombo vyote vya ulinzi na usalama kwasababu Jeshi la Polisi linaenda kwenye mradi mpya unaoitwa majiji salama utakaowezesha kufunga mitambo ya Kamera za kisasa 6500 kama ilivyoelezwa kwenye Bajeti ya Fedha ya Jeshi la Polisi 2024/25 ya kuhakikisha haya majiji manne yako salama ikiwa ni awamu ya kwanza ”Alisema Mhe. Sillo

Aidha, Naibu Waziri Sillo, katika hatua nyingine amekemea na kuelekeza Jeshi la Polisi Nchini kusimamia suala la kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia pamoja na mauaji huku akiitaka jamii pia kubadilika na kurudi kwenye maadili ya Kitanzania kwa kushirikiana na kamati za ulinzi na usalama kwenye maeneo yao kwa kuwafichua wahalifu wa aina hiyo.

“Ndugu zangu Watanzania hakuna utajiri au mali zinazopatikana kwa njia ya kufanya ukatili au mauaji hivyo niwasihi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na ambazo hazivunji sheria na taratibu za nchi kwani utajiri wa halali na wa amani unapatikana kwa kufanya kazi tu nasi vinginevyo” Alisema Mhe. Sillo

Katika Mkutano huo Mhe. Sillo amezielekeza Idara za Uhamiaji na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) nchini kushirikiana kuhakikisha Vitambulisho hivyo vinatolewa kwa Watanzania halali na kwa usahihi kwa kufuata kanuni na taratibu za nchi bila kushinikizwa kutumika na wanasiasa ambao hawana nia nzuri.

Kwa upande wake Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa Kagera, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Brasius Chatanda kwa niaba ya Viongozi wote waliohudhuria Mkutano huo kutoka Idara mbalimbali amemuahidi Naibu Waziri Sillo kuwa, maelekezo na miongozo yote wameipokea kwa utekelezaji na kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuvipambambania Vyombo vya Usalama kwa kuboresha mazingira ya kazi na kuahidi kufanya kazi kwa weledi.

”Mhe. Naibu Waziri kwa niaba ya wenzangu wote itoshe kusema maelekezo na miongozo uliyoitoa ndio dira katika utendaji kazi wetu tumeipokea na tunaenda kwenye utekelezaji wa haraka iwezekanavyo kwani kila Idara iko imara” Alisema Kamanda Chatanda

Related Posts