Mapema siku ya Alkhamis (Agosti 1), Ayatullah Ali Khamenei aliongoza sala ya jeneza mjini Tehran, kabla ya maiti ya Haniyeh kupelekwa nchini Qatar kwa maziko baada ya sala ya Ijumaa.
Maelfu ya waombolezaji walikusanyika wakiwa wamebeba mabango yenye picha za Haniyeh na bendera za Palestina katika Chuo Kikuu cha Tehran kabla ya sala hiyo kuanza, huku wakipaza sauti za kuzilaani Israel na Marekani.
Soma zaidi: Baraza la Usalama la UN laijadili hali ya Mashariki ya Kati
Televisheni ya taifa ya Iran ilionesha majeneza ya Haniyeh na mlinzi wake yakiwa yamefunikwa bendera ya Palestina wakati wa sala hiyo iliyohudhuriwa pia na maafisa wa ngazi za juu wa Iran, akiwamo Rais Masoud Pezeshkian na mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi, Jenerali Hussein Salami.
Miito ya kulipiza kisasi
Kwenye sala hiyo, mkuu wa sera za nje wa Hamas, Khalil al-Hayya, aliapa kwamba ujumbe wa Haniyeh ungeliendelea kuishi na kwamba wangelikabiliana na Israel hadi watakapoing’owa “kutoka kwenye ardhi ya Palestina.”
Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Bagher Ghalibaf, alisema kwamba nchi yake ingeliitekeleza amri ya kiongozi mkuu Khamenei, akimaanisha kulipiza kisasi mauaji ya Haniyeh. “Ni jukumu letu kujibu mauaji haya kwa wakati muafaka na mahala muafaka.” Alisema spika huyo.
Soma zaidi: Miito ya kulipiza mauaji ya Haniyeh yatolewa katika mazishi yake
Mara tu baada ya mauaji hayo kutangazwa siku ya Jumatano (Julai 31), Ayatullah Khamenei alisema kwamba “ulikuwa ni wajibu wa Iran kulipiza kisasi kwa damu ambayo imemwagwa ndani ya ardhi ya Iran.”
Gazeti la New York Times liliwanukuu maafisa wa Iran wakisema kwamba Khamenei ameamuru nchi yake kuishambulia moja kwa moja Israel.
“Mazayuni hivi karibuni watayashuhudia matokeo ya tendo lao la woga na la kigaidi.” Alisema Rais Pezekshian, ambaye alikuwa kiongozi wa mwisho wa ngazi za juu wa Iran kukutana na Haniyeh siku ya Jumanne kabla ya kuuawa kwake.
Haniyeh alikuwa ziarani nchini Iran kuhudhuria kuapishwa kwa Pezekshian.
Guterres aonya hatari ijayo
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, alisema mashambulizi hayo mjini Tehran na yale ya Beirut, yaliyomuua kamanda mkuu wa kundi la Hizbullah, Fouad Shukr, yalikuwa “muendelezo wa hatari wa vita.”
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilikutana kwa dharura siku ya Jumatano kujadili tukio hilo kwa ombi la Iran.
Kwenye mazungumzo yao kwa njia ya simu, mawaziri wa mambo wa kigeni wa Misri na Jordan waliishutumu Israel kwa kuchochea hali kuwa mbaya zaidi.
Soma zaidi:Je Kiongozi wa Hamas, Ismail Haniyeh ni nani?
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani, Antony Blinken alitoa wito kwa pande zote kujikita kwenye kukomesha mapigano.
Hata hivyo, Waziri Mkuu wa Qatar, Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al-Thani, amesema mauaji ya Haniyeh yameutia mashakani mchakato mzima wa kusaka makubaliano ya kusitisha mapigano.
Qatar ndiyo inayoongoza vikao vya majadiliano ya kusitisha mapigano, ambavyo kwa upande wa Hamas vilikuwa vikiongozwa na Haniyeh.
Vyanzo: Reuters, AFP