AKILI ZA KIJIWENI: Simba isilaumiwe kumkosa Elie Mpanzu

SIMBA ilipambana sana kuisaka saini ya winga machachari wa AS Vita, Elie Mpanzu lakini kuna wakati jitihada huwa hazizai matunda na ndicho kimetokea kwao.

Walifanikiwa kwa kiasi kikubwa kumshawishi mchezaji ajiunge nao kwa kumpa ahadi ya masilahi mazuri na mchezaji akatamani kuwa sehemu ya kikosi chao.

Shida ikaja kwa AS Vita ambayo ilionyesha kubadilika badilika katika kuamua hatima ya mchezaji huyo na danadana zao ziliashiria hawakuwa na mpango wa kumuuza Mpanzu kwenda Simba.

Kwanza walitaka dau ambalo Simba ilikuwa tayari kulilipa lakini baadaye ghafla wakadai kuna changamoto ya umiliki wa mchezaji huyo hivyo Simba ili impate inatakiwa kuongeza fedha.

Kwa vile Simba ilikuwa na uhitaji mkubwa wa Mpanzu ikawa tayari kulipa hata hilo dau la pili ambalo AS Vita walilihitaji lakini timu hiyo ya DR Congo ikaanza kuwazungusha kwa kutoa sababu nyingi ambazo hazikuwa zinaeleweka.

Mwishowe Simba iliamua kunyoosha mikono juu na kuwaachia AS Vita Club mchezaji wao kwa vile ilionekana klabu hiyo ya DR Congo haiko siriazi na haionyeshi utayari wa kumwachia Mpanzu.

Mara ghafla tumesikia Mpanzu ameenda Ubelgiji na sasa yupo katika hatua za mwisho za kukamilisha uhamisho wa kujiunga na KRC Genk inayoshiriki Ligi Kuu nchini humo.

Inavyoonekana ni kama AS Vita ilikuwa inafahamu kinachoendelea juu ya Mpanzu hasa kwa suala la kuhamia Genk na ndiyo maana ikawa inawazuga Simba kwa kuwapa masharti tofauti mara kwa mara.

Ila kiungwana ingewachana mapema tu ili watafute opsheni nyingine kuliko kuwachelewesha hadi muda wa usajili wa wachesaji kwa ajili ya mashindano ya klabu Afrika ulipoisha.

Related Posts