Waswahili wanasema mtaka cha uvunguni shurti ainame, na vijana wa sasa wanasema anaweza inua kitanda, uchaguzi ni wako, uiname au uinue kitanda… hebu twende pamoja.
Kwa muda mrefu nimekuwa nikisikia watu wakitofautiana wanasema huyu hana akili mpuuze tu. Wazazi nao wanasema huna akili kama mama au baba yako!
Hii ikanifanya nijiulize swali, hivi akili ni nini? Na nini kinafanya mtu awe na akili na mwingine asiwe nazo?
Kazi ya kutafuta maana ikaanza, ninaangalia kwenye vitabu na maana za kawaida mtaani, watu wanasema kuwa na akili ni kufaulu darasani na maishani au kufanya kazi nzuri, wengine wakaniambia ni kuwa na uwezo wa kufanya mambo kijanja.
Naam, wengine wakasema akili ni kichwa chepesi, sijui kwako akili ni nini. Hata hivyo, hata ukishindwa kujua maana yake nina hakika unafahamu fika nani hana, nani anazo na nani anajizima data.
Akili kwa Kiingereza inaitwa ‘intelligence’ na hupimwa kwa kipimo maalumu tunachokiita kipima akili (IQ test). Kipimo hiki huweza kupima uwezo wa kuchakata mambo na taarifa kadhaa katika muda maalumu.
Ubongo ndio chimbuko la akili, ubongo jinsi ulivyo ndio kiungo na chanzo cha uwezo ulionao na pengine ndio akili zenyewe.
Wengine wamesema ubongo unaochaji sana wakimaanisha akili nyingi.
Ubongo huundwa kuanzia wiki ya nne ya ujauzito, yaani kabla hata mtu hajafahamu ana ujazito tayari. Kazi ya kuunda ubongo imeanza, jinsi ubongo unavyochakata mambo ndio akili zenyewe, hivyo naweza kusema akili zinaanza kuundwa wiki ya nne.
Uko msemo wa Kiswahili usemao ukubwa wa pua sio wingi wa kamasi, au ukubwa wa kichwa sio ukubwa wa ubongo au wingi wa akili.
Hata hivyo, kuna uhusiano mkubwa na kiwango cha ubongo, akili na ukubwa wa kichwa, ubongo hukamilika, kutengenezeka na kichwa kufunga utosi miaka miwili hivi.
Ndani ya fuvu la kichwa kulikofichwa ubongo uongozao maisha, kuna lazimu kuwe na uwiano unaokubalika kati ya ubongo na maji, kimoja kisizidi chenzake, ubongo ni mkusanyiko wa mamilioni ya chembe chembe ambazo idadi yake haipungui ama kuongezeka na hazizaliwi tena, hivyo zikiharibika zimeharibika.
Ubongo huanza kupokea mafunzo na mafundisho kutoka kwa wazazi, jamii na walimu wa kila aina na mazingira yanayomzunguka mtoto.
Naam, kadiri mtoto atakavyokua na kuwa kijana ubongo wake hukaa katika kiwango cha ukubwa stahiki kwa uwiano wa fuvu lake, lakini uzee huja na ubongo hupungua. Kama unavyokua pia huzeeka na pengine ni vivyo hivyo kwa akili.
Dunia inatafuta watu wenye akili, wanaofikiri vizuri na kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, jamii inataka watu imara wanaokabili changamoto wanazozipitia, wenye uwezo wa kuchakata mambo. Watu wasio na akili hawafurahiwi kabisa na wanatengwa na jamii. Hivyo ni muhimu kuwa na akili tena zenye akili.
Sababu ya kuwa na akili nyingi
Kurithi kutoka kwa wazazi, haturithi weupe au weusi pekee au kimo tu. Tunarithi akili pia, wazazi wenye akili huzaa watoto wenye akili na pengine nichelee kusema ni miujiza pekee tu kwa wasio na akili kuzaa wenye akili.
Hivyo chagua mzazi mwenza mwenye akili ili muwe na watoto wenye akili, kanuni ya mtoto wa nyoka ni nyoka ni dhahiri katika hili. Usitegemee maembe kwenye mti wa mchungwa.
Lishe bora katika siku 1,000 za kwanza za mtoto. Tunaanza kuhesabu siku hizi tangu siku ya kwanza ya mimba mpaka miaka miwili. Hapa tunataka mama ale mlo kamili wenye virutubisho muhimu, mwili haujengwi kwa tofali na akili haziji kwa kuchomea chuma kwa gesi, mzazi ale mlo kamili, mtoto ale mlo kamili.
Kula vyakula vya kuujenga mwili, vyenye vitamini na madini muhimu. Jitahidi usikose madini ya chuma, vitamin Bs, folic na iodine, haya ni muhimu sana kwenye akili. Kula virutubisho sio kujaza tumbo.
Mtoto akichelewa kulia, akili nazo zinachelewa kabisa, mtoto akinywa maji wakati wa kujifungua mambo haya huchangia mno uimara wa ubongo.
Afya bora, kuepuka maradhi ya mara kwa mara na homa kama homa ya uti wa mgongo, maradhi ya syphilis, surua na mengine mengi, hata kifafa yanachangia sana kudumaza ubongo.
Pia ajali ya kichwa kwa aina zake, epuka maradhi na ajali kwa watoto, zuia kabisa inapowezekana. Zingatia ushauri wa wataalamu.
Hewa safi na damu ya kutosha, ubongo huhitaji oxygen kutekeleza majukumu yake.
Hufanya kwa ufanisi katika shinikizo la ubongo stahiki, hivyo kuwa na hewa safi, kuwa na damu ya kutosha kwa msukumo unaotakiwa.
Nitataja sababu nyingine nyingi zinazochochea ukuaji wa akili ya mtoto, ikiwa ni pamoja na kucheza sana, kuuliza maswali na kupata majibu sahihi wakati mwingine.
Nimalize na kipima akili IQ, watu wenye maksi 75 kushuka chini huhesabiwa hawana akili sawa sawa, wana mtindio wa ubongo, kati ya 76 na 115 hawa wana akili wastani, na ndio wengi duniani, wenye IQ kati ya 116 na 140 hawa wana akili za juu na wengi wamepewa jina la majiniasi, wako watu konki wenye kati ya 146 na 200, hawa wana uwezo wa juu mno.
Sijui wewe una ngapi au mtoto wako ana ngapi, ninajua wako wenye 20 na wenye 180, sasa fahamu inawezekana kuboresha huo uwezo wako, wekeza muda kwenye kuinua akili yako, wewe unayesoma haya kwenye simu yako unaweza kabisa.
Albert Einstein, mwanasayansi mashuhuri wa karne ya 20 alipofariki, wataalamu waliiba ubongo wake na kuuchunguza kuona kama ulikuwa wa tofauti na wanadamu wengine, maana alikuwa na IQ kati ya 160-170 licha ya nadharia nyingi za wasomi kadhaa, wote wamekubaliana kuwa alikuwa na ubongo mkubwa kuliko wastani.
Mwandishi ni Daktari Bingwa wa upasuaji Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dodoma. Kwa maswali, maoni na majibu muandikie [email protected]