Rais Samia awapa mbinu wamiliki wa mabasi kukabili ushindani wa SGR

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema licha ya athari zilizoanza kujitokeza kwa wamiliki wa mabasi na malori, bado Tanzania ina fursa nyingi za wasafirishaji hao kunufaika.

Msingi wa kauli ya mkuu huyo wa nchi ni kile alichoeleza, kuanza kwa mradi wa treni ya umeme ya abiria kwa namna fulani kumesababisha kupungua kwa mabasi barabarani katika njia unakopita mradi huo.

Amesema hali kama hiyo inatarajiwa katika usafirishaji wa mizigo kwa malori, pale treni hiyo itakapoanza kusafirisha.

Pamoja na athari hizo, Rais Samia amesema bado wasafirishaji hao wana fursa ya kunufaika hasa katika njia nyingine ambazo mradi huo haujafika.

Rais Samia ameyasema hayo leo Alhamisi Agosti 1, 2024 alipozungumza na vyombo vya habari akiwa ndani ya treni ya SGR kuelekea Stesheni ya Pugu, ikiwa ni uzinduzi wa safari za treni ya umeme kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma.

Hata hivyo, amesema kupungua kwa mabasi barabarani inaweza kuwa athari mbaya kwa wafanyabiashara lakini nzuri kwa Serikali kwa kuwa itapunguza ajali.

“Hasara moja ambayo imeanza kuonekana ni kupungua kwa mabasi barabarani, kwa wafanyabiashara ni mbaya lakini kwa nchi ni nzuri kwa sababu inapunguza ajali pia na sasa usafiri barabarani unadhibitiwa vizuri,” amesema.

Hata hivyo, ameeleza bado wasafirishaji hao hawataathirika kwa kuwa kuna njia nyingine treni hiyo haijafika na hivyo wanayo nafasi ya kupeleka mabasi huko.

“Lakini sasa wanapunguza mabasi eneo moja ambalo tayari kuna maendeleo haya, lakini Tanzania ni kubwa kuna maeneo ambayo yanahitajika kwa hiyo sasa yatakwenda kule,” amesema.

Athari pia, amesema zitashuhudiwa katika usafirishaji wa mizigo kupitia malori, hasa pale ambapo treni hiyo itaanza kubeba mizigo, lakini bado kutakuwa na maeneo ambayo hayatakuwa na mradi huo.

Katika maungumzo yake akiwa ndani ya treni kutoka stesheni ya Posta kwenda ile ya Pugu, mkuu huyo wa nchi ameeleza furaha yake ya kufanikiwa kukamilisha miradi waliyoanzisha akiwa na mtangulizi wake, Hayati John Magufuli.

“Nina faraja kusema kwamba yale ambayo niliyaanza na mwenzangu marehemu (Magufuli) nimeyakamilisha kwa hiyo ni miradi ambayo kwa Tanzania ni muhimu sana,” amesema.

Hata hivyo, aliusifu uamuzi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuanza safari za kwenda Dodoma Julai 25, mwaka huu akisema alivyoona alifurahia, akidokeza: “(Kadogosa, Mkurugenzi Mkuu wa TRC) alikuwa anaogopa kutumbuliwa.”

Katika hatua nyingine, amesema hautazami mradi huo kwa sura ya kibiashara pekee, bali wakati mwingine anautazama kama huduma kwa kuwa una manufaa katika maeneo mengine.

Sababu ya kupambania utekelezwaji wa mradi huo ni kile alichoeleza, analenga kuiunganisha Tanzania na mataifa ya Burundi na Jamhuri ya Demokrasi ya Congo ili kupata soko la bidhaa.

Amesimulia zamani aliwahi kupanda treni la awali (MGR) kutoka Dar es Salaam hadi Moshi na akiwa njia alikumbwa na changamoto lukuki likiwemo vumbi.

“Hadi kufikia hatua iliyofikiwa sasa namshukuru Mungu na kwamba namuomba Mungu njia yote imalizwe hadi kufikia Burundi,” amesema.

Related Posts