MAKOCHA 17 wa mchezo wa kikapu nchini wanashiriki katika mafunzo ya mchezo huo, yanayoendelea katika kituo cha michezo cha Jakaya Mrisho Kikwete (JMKYP).
Mafunzo hayo yanayomalizika kesho Jumamosi, yameandaliwa na shirikisho la mchezo huo nchini (TBF) kupitia kamisheni ya makocha.
Akiongea na Mwanaspoti katika viwanja vya JMKYP, kamishina wa makocha wa TBF, Robert Manyerere alisema mafunzo hayo yanatolewa na wakufunzi wa ndani ambao ni Bahati Mgunda, Ashrafu Haruni pamoja na yeye mwenyewe.
Alisema katika mafunzo hayo, makocha hao wamekuwa wakiingia darasani kila siku na baada ya hapo wanafanya uwasilishaji kwa vitendo ‘presentation’.
“Baada ya hapo, makocha hawa wanaingia uwanjani kufanya kwa vitendo na siku ya mwisho ya mafunzo kesho (Jumamosi) watafanya mitihani,” alisema Manyerere.
Alisema makocha wanaopata mafunzo wanatoka Geita, Magu, Mvomero, Itigi, Unguja, Mpwapwa, Dodoma mjini, Mtwara, UDSM Outsiders, Kigamboni herous, Mambo basketball, Pazi Queens na Uhamiaji.
Manyerere alisema mafunzo hayo yanatolewa kwa pamoja ‘Level one na two’.
Akizungumzia kuhusu mipango yao ya baadaye, alisema wanakusudia kuendesha kozi katika mtandao.