AKILI ZA KIJIWENI: Somo lingine tunalipata kwa Dulla Makabila

NDUGU yetu Dulla Makabila amekosa kirahisi fursa ya kupiga shoo kwenye kilele cha tamasha la Simba Day, keshokutwa Jumamosi.

Kilichomponza ni mdomo wake mwenyewe ambao siku moja ulitoa maneno yasiyo na staha kwa Simba muda mfupi baada ya kutangaza amehamia Yanga.

Jamaa baada ya kipindi fulani kutangaza kuhamia Yanga, aliibeza Simba kwa maneno mengi ya nyodo jambo ambalo halikuwafurahisha mashabiki wa timu hiyo.

Kumbe walimuweka kiporo bwana na kumbukumbu hiyo ya maneno ya Dulla Makabila ikabaki vichwani mwao wanasubiria siku tu ya kulipa kisasi.

Sasa jamaa amenasa kwenye mtego wao baada ya kusikia ni miongoni mwa wasanii watakaopanda stejini Simba Day kutumbuiza, mashabiki wamecharuka nchi nzima dhidi yake.

Wameupa agizo uongozi wao kuwa usithubutu kumpa Makabila fursa ya kupiga shoo siku hiyo na kama wakifanya hivyo basi kitakachomtokea wasije kulaumiwa.

Kwa vile mashabiki ndio mabosi wa Simba Day, uongozi wa timu hiyo umewasikiliza na ukawapa ahadi mwanamuziki huyo hawezi kupewa nafasi ya kupanda jukwaani siku ya kilele cha tamasha hilo.

Kinachomtokea Makabila kiwe somo kwa wasanii na wanamuziki wetu, wawe wanaweka akiba ya maneno pale wanapopata fursa fulani.

Kutoa kauli zisizofaa kwa watu wasiohusika na shoo yako sio jambo zuri kwani siku moja utawahitaji na watashindwa kukupa sapoti kama ilivyotokea kwa ndugu yetu Dulla Makabila.

Related Posts