POLISI WAONYA MATAPELI WANAOJIFANYA WATUMISHI WA UMMA ZANZIBAR – MWANAHARAKATI MZALENDO

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharib, Kamishna Msaidizi wa Polisi Abubakar H. Ally, ametoa onyo kuhusu matapeli wanaojifanya watumishi wa umma na kuwatapeli wananchi kwa ahadi za ajira za serikali. Akizungumza ofisini kwake Madema, Zanzibar, Kamanda Abubakar alieleza jinsi mtuhumiwa mmoja alivyokuwa akiwatapeli wananchi kwa kujifanya mtumishi wa umma na kuahidi kuwapatia ajira za Vikosi Maalum vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Katika taarifa yake, Kamanda Abubakar alisema kuwa mnamo tarehe 22/07/2024, mtuhumiwa huyo alimtapeli mwananchi fedha za shilingi 1,400,000 (milioni moja na laki nne) akidai kuwa yeye ni mtumishi wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) na kwamba angeweza kumsaidia kupata ajira katika idara hiyo, ingawa alijua kuwa jambo hilo lilikuwa kosa.

Kamanda Abubakar alifafanua kuwa mtuhumiwa amekuwa akitumia mbinu za kuwa karibu na ofisi za serikali ili kuaminisha wahasiriwa kuwa ni mtumishi halali wa taasisi hizo, na baada ya kufanikisha utapeli huo, hutoweka mara moja.

Akiwaomba wananchi kuwa waangalifu, Kamanda Abubakar alitoa wito kwa watu katika kipindi hiki ambapo Mkuu wa Jeshi la Polisi, Afande IGP. Camillus Wambura, ametangaza usaili kwa vijana waombaji ajira za Jeshi la Polisi, kuchukua tahadhari dhidi ya matapeli wanaotumia fursa hii kwa njia za udanganyifu.

Aidha, Kamanda Abubakar aliwataka wananchi wote waliopata kadhia ya kutapeliwa kufika kituo cha Polisi Madema ili kumsaidia kutambua mtuhumiwa huyo na kusaidia katika uchunguzi wa kesi hiyo.

 

#KonceptTvUpdates

Related Posts