Sungusia akerwa mawakili kupigwa ‘Tanganyika jeki’ na polisi hadharani

Dodoma. Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Haroad Sungusia amemwomba Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko kusema neno kuhusu baadhi ya mawakili kunyanyaswa na polisi kwa kupigwa Tanganyika jeki mbele ya wateja wao, jambo alilosema linashusha heshima ya taaluma hiyo.

Sungusia ameyasema hayo leo Jumatano, Agosti Mosi, 2024 wakati wa Mkutano Mkuu wa TLS unaofanyika jiji Dodoma.

Amesema kuna wakati kumekuwa na mivutano kati polisi na mawakili ambapo kuna wakati ambapo mawakili wamekuwa wakikamatwa bila kufuata utaratibu au pasipokuwa na nafasi ya kuwajulisha wenzao kuwa wamekamatwa.

Pia, amesema mawakili wamekuwa wakikamatwa pasipokuambiwa makosa yao na wakati mwingine wakichanganywa na wateja wao.

“Tunaona katika kipindi hiki wimbi la kukamata mawakili limeanza kupungua kwa kasi sana na tunaamini kuwa jambo hilo litakwisha na halitakuwepo tena katika Jamuhuri ya Muungano na mawakili watakuwa na heshima yao,” amesema.

Sungusia amesema utaratibu wa kushughulikia nidhamu za mawakili unajulikana pasipo kuwa na sababu ya mvutano kati ya mawakili na wasimamizi wa sheria.

“Tunaomba useme neno moja tu kwa vyombo vya usimamizi wa sheria bila shaka heshima ya mawakili unaowaona mbele yako itaweza kuboresha inakuwa jambo la kusikitisha sana mheshimiwa mgeni rasmi unaenda mahakamani mbele ya mteja wako unashikwa tanganyika jeki,” amesema.

Amesema ofisi za mawakili zinafahamika na wana anwani zinazofahamika na wamekuwa wakishirikiana na TLS pale ambapo anapohitajika aweze kuripoti mahali hapo.

Sungusia amesema kuwa wameendelea kujisimamia nidhamu ya mawakili.

Aidha, amesema jukumu la kutetea na kulinda haki za watu inahitaji miundombinu bora ya haki ambayo inazingatia kwa dhati utawala wa sheria na uhuru wa mahakama.

“Kwa sababu hiyo TLS inaomba Serikali iendelee kuwahimiza viongozi wa kisiasa waendelee kuheshimu uhuru wa mahakama na kujizuia kufanya vitendo ambavyo au kauli ambazo kwa njia moja ama nyingine zinaweza kuashiria kukiuka ama kuminya uhuru wa Mahakama na utawala wa sheria,” amesema.

Amesema wao kama mawakili ni maofisa wa mahakama na hivyo wamekuwa wakichukua hatua za kulinda na kutetea maadili yao pamoja na kusimamia utawala wa sheria.

“Ikiwa viongozi mbalimbali wataheshimu utawala wa sheria tunaamini kuwa itakuwa ni rahisi sana kuiga utawala wa sheria na kufanya hivyo tutaweza kudumisha haki ambayo ni mlezi wetu mkuu wa amani,”amesema.

Ametaja pia changamoto iliyokikuta chama hicho kutishiwa kufutwa katika kipindi cha kati ya mwaka 2016 na 2017.

Amewashukuru wabunge na wadau mbalimbali kwa kutochukua hatua hiyo na chama hicho kimeendelea kuwepo hadi leo ambapo kimetimiza miaka 70 kikiwa na mategemeo ya kwenda zaidi.

Akijibu hoja ya kukamatwa bila staha, Naibu Waziri na Waziri wa Nishati Dk Doto Biteko aliyemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan amesema nchi inaendeshwa kwa utawala wa sheria na imani yake kuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Pindi Chana amelisikia na kulichukua.

 “Basi tutakapokutana mwakani hili lisiwe changamoto ya kusema sana tuwe tumelitafutia majibu kwa sababu kweli mawakili hawa wanakuja kuwatetea watu na wakati mwingine kama wanavyojiita maofisa wa mahakama ni muhimu wapate heshima yao,” amesema.

Related Posts