Wauza nyama wagoma, wananchi wahaha kusaka kitoweo Iringa

Iringa. Wafanyabiashara wa nyama katika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa leo Alhamisi Agosti Mosi, 2024 wamegoma kufungua mabucha yao wakilalamikia kupanda kwa tozo na ushuru wa uchinjaji.

Tozo hizo wanadai zinatozwa na Halmashauri ya Manispaa ya Iringa na wamechukua hatua hiyo ili kuushinikiza uongozi upunguze gharama hizo walizodai zimepanda kutoka Sh4,000 mpaka Sh10,000.

mmoja wa wauzaji wa nyama eneo la Iringa Mjini, Jackson Mwacha amesema sababu kubwa ya kufunga mabucha ni kupanda kwa gharama ya ng’ombe na tozo za halmashauri.

Amebainisha kuwa bei ya ng’ombe wa kawaida imepanda kutoka Sh700,000 na kufikia Sh1 milioni, hali inayosababisha hasara kwenye biashara hiyo.

Mwenyekiti wa umoja wa wachinjaji, Salehe Msungu amesema walipokea taarifa ya kupanda kwa ushuru wiki moja iliyopita, licha ya juhudi za kutaka majadiliano na ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa, hawajapata mafanikio.

Mgomo huo umeathiri biashara zingine, kama vile wauzaji wa nyanya, vitunguu, viungo na vifungashio, wateja wao wamepungua baada ya mabucha kufungwa.

Elisha Kivike, mpenzi wa ugali na nyama, amesema kukosekana kwa nyama kumeathiri mlo wake wa kawaida, akilazimika kutumia mboga za majani tofauti na alivyozoea.

Baadhi ya Mama Lishe mjini Iringa, akiwamo  Asia Miho amesema biashara ya chakula imekuwa mbaya kwa siku ya leo.

Amesema wateja wake wengi hupendelea kitoweo cha nyama kuliko vingine.

“Bila nyama, biashara haiendi, watu wengi hupendelea nyama kuliko mboga nyingine, leo tumekomeshwa,” amesema Miho.

Akizungumza na Mwananchi Digital kwa simu, Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Ibrahim Ngwada amekiri kuwepo kwa mgomo huo na kuthibitisha kupanda kwa tozo hizo kutoka Sh4,000 hadi Sh10,000.

Hata hivyo, amesema kwa sasa wameanza majadiliano na wafanyabiashara wa nyama, na wamekubaliana kuendelea na bei ya tozo za zamani hadi halmashauri itakapopitia upya tozo hizo.

Related Posts