Iran na washirika wajadili kisasi cha mauaji ya Haniyeh – DW – 01.08.2024

Vyanzo vitano tafauti vililiambia shirika la habari la Reuters kuwa mkutano huo wa siku wa Alkhamis (Agosti 1) mjini Tehran ulitazamiwa kuhudhuriwa na wawakilishi wa makundi ya Islamic Jihad na Hamas kutokea Palestina, Houthi kutoka Yemen, Hizbullah kutoka Lebanon na makundi ya wanamgambo kutoka Iraq. 

“Iran na wajumbe wa Mshikamano wa Mapambano watakuwa na kikao cha tathmini ya kina ili kupata njia bora zaidi na yenye ufanisi zaidi ya kulipiza kisasi dhidi ya utawala wa Kizayuni.” Afisa mmoja mwandamizi wa serikali ya Iran aliye karibu na mkutano huo aliliambia Reuters.

Soma zaidi: Khamenei aongoza sala ya jeneza la Haniyeh

Afisa mwengine wa serikali ya Iran alisema kiongozi mkuu wa Iran, Ayatullah Ali Khamenei, pamoja na wajumbe wa ngazi za juu wa Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi walitazamiwa kuhudhuria mkutano huo. 

Mkuu wa Majeshi wa Iran, Jenerali Mohammad Baqeri, alikiambia kituo cha televisheni ya serikali kuwa nchi yake inashirikiana na washirika wake kupanga jinsi watakavyolipiza kisasi mauaji ya Haniyeh, huku akisisitiza kwamba “utawala wa Kizayuni utajutia.”

Vita vinanukia?

Iran na Hamas zinaishutumu Israel kufanya mashambulizi yaliyomuua Haniyeh masaa kadhaa baada ya kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa rais mpya wa Iran, Masoud Pezekshian, usiku wa kuamkia jana Jumatano kaskazini mwa mji mkuu wa Iran, Tehran.

Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatullah Ali Khamenei, akiongoza sala ya jeneza la Ismail Haniyeh mjini Tehran.
Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatullah Ali Khamenei, akiongoza sala ya jeneza la Ismail Haniyeh mjini Tehran.Picha: Iranian Leader Press Office/Anadolu/picture alliance

Hata hivyo, maafisa wa Israel hawajatoa tamko lolote rasmi la kukubali kufanya mauaji hayo, lakini mkuu wa jeshi lake la anga, Tomer Bar, alisema siku ya Jumatano (Julai 31) kwamba wako tayari kukabiliana na yeyote anayepanga kuwadhuru raia wa Israel.

Soma zaidi: Blinken aitaka Mashariki ya Kati kujizuia kuongeza mzozo

 “Tuko tayari kwa kujilinda. Mamia ya wanajeshi wa anga pamoja na maafisa wa ardhini wamewekwa kote nchini wakiwa na mifumo bora kabisa ya ulinzi, tayari kutekeleza majukumu yao.” Alisema Bar.

Lufthansa yafuta safari za Tel Aviv

Wakati hayo yakijiri, shirika la ndege la Ujerumani, Lufthansa, lililazimika kufuta safari zake kutoka Cyprus kwenda Tel Aviv kwa sababu za kiusalama. 

Bango lenye picha ya marehemu Ismail Haniyeh.
Bango lenye picha ya marehemu Ismail Haniyeh.Picha: IMAGO/NurPhoto

Ndege chapa A321 iliyokuwa imetuwa uwanja wa ndege wa Larnaca ikitokea Munich kuelekea Tel Aviv ilitakiwa kufuta safari yake, baada ya Iran kutangaza kwamba ingelifunga anga lake kwa muda mapema asubuhi ya Alkhamis.

Soma zaidi: Miito ya kulipiza mauaji ya Haniyeh yatolewa katika mazishi yake

Ndege nyengine inayomilikiwa na kampuni mwenza ya Lufthansa nchini Austria, nayo pia ililazimika kubadilisha safari yake na kutuwa mjini Sofia, badala ya Tel Aviv. 

Hata hivyo, kufikia jioni ya Alkhamis, msemaji wa Lufthansa alisema kwamba kwa sasa hakuna zuio tena la ndege kuelekea Israel.

Vyanzo: dpa, Reuters

Related Posts