Dk. Yonazi awataka viongozi kufanya kazi kwa weledi kufikia malengo

Na Mwandishi Wetu, Arusha

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu, Dk. Jim Yonazi amewataka viongozi wa ofisi hiyo kufanya kazi kwa weledi ili kufikia malengo ya Serikali katika kuwahudumia Watanzania.

Ameyasema hayo leo Agosti Mosi,2024 jijini Arusha alipohitimisha kikao cha mazingativu (Retreat) kilichohusisha viongozi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Menejimenti, Watumishi na taasisi zilicho chini ya ofisi hiyo.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dk. Jim Yonazi, akigawa vyeti kwa viongozi wakati wa kikao cha Mazingativu kinachohusisha menejimenti ya ofisi hiyo, watumishi na taasisi zilizo chini yake kilichofanyika jijini Arusha.

Alisema ana imani kubwa kwa watumishi na viongozi wa ofisi hiyo kuwa watakuwa wenye thamani na utulivu na wenye nia ya kuwatumikia Watanzania kwa weledi na moyo thabiti.

“Sisi hapa wengi ni viongozi, watu wa chini yetu ndio wametuwezesha kuwa viongozi hivyo, tumesiweke mazingira magumu kwa waliopo chini yetu katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku,” amesema Dk. Yonazi.

Dk. Yonazi amewashukuru viongozi wa juu wa ofisi hiyo kwa maandalizi mazuri ya kikao hicho kilichokuwa na lengo la kuendeleza mafunzo kazini kuwaleta watumishi na viongozi pamoja kwa ajili ya kujifunza na kuwa na mbinu ambazo zitaboresha utendaji wa shughuli za kila siku za ofisi.

Awali akizunguza katika kikao kazi hicho Mkurugenzi wa Mipango na Bajeti kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Eleuter Kihwele, amesema mafunzo hayo ambayo yalishafanyika mwaka 2023 yamesaidia katika kuboresha utendaji kazi na kuimarisha umoja kwa kuwaleta pamoja watumishi wote.

Amesema utendaji wa pamoja kwa maana ya viongozi na watumishi kukaa kujadili pamoja kunachochea ufanisi kazini na kuyafikia malengo yaliyokusudiwa.

Related Posts