Migomo ya wafanyabiashara, Tume yapewa zigo hili..

Dar es Salaam. Licha ya baadhi ya wadau kupongeza hatua ya Rais Samia Suluhu Hassan kuunda Tume ya Rais ya Kutathmini na Kushauri kuhusu Masuala ya Kodi, wametaka tume hiyo ihusishe walengwa wanaolalamikia mifumo ya kodi.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu iliyotolewa jana Jumatano, Julai 31, 2024, tume hiyo imeundwa na viongozi tisa wakiongozwa na Balozi Ombeni Sefue ambaye ni mwenyekiti.

Balozi Sefue, Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu atawaongoza wajumbe hao wenye utaalamu ya masuala ya kodi.

Rais Samia ameunda timu hiyo ikiwa ni siku nne zimepita tangu kuahidi kufanya hivyo akiwa katika mkutano na Baraza la Taifa la Biashara Tanzania (TNBC) uliofanyika Ikulu, jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Rais Samia, tume hiyo pia itachunguza na kubaini changamoto za utekelezwaji wa sera na sheria katika mifumo hiyo, huku akiahidi ingehusisha wajumbe kutoka serikalini na sekta binafsi, ili kupendekeza mfumo stahiki wa kikodi unaoendana na Tanzania.

Msingi wa uamuzi huo ni malalamiko ya wafanyabiashara kuhusu changamoto katika mifumo ya kikodi iliyopo, ambayo kimsingi imekuwa shubiri kwao na kusababisha migomo.

Mbali na Balozi Sefue, wajumbe  wengine katika tume hiyo ni aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Florens Luoga ambaye amewahi pia kuwa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Wengine ni aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad na aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Price Water House Coopers (PwC) Tanzania, Leonard Mususa.

Wengine ni Aboubakar Mohamed Aboubakar,mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU), Balozi Mwanaidi Sinare Maajari ambaye ni mshauri wa masuala ya sheria.

Wajumbe wengine ni David Tarimo, mtaalamu na mshauri wa masuala ya kodi na aliyekuwa mkuu wa Idara ya Ushauri wa Kodi, PwC.

Pia yumo Balozi Maimuna Tarishi, Katibu Mkuu mstaafu na Rished Bade ambaye ni Kamishna wa Fedha za Nje, Wizara ya Fedha ambaye pia aliwahi kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Wataka tume iwe shirikishi

Akizungumza na Mwananchi leo Agosti mosi, 2024, mfanyabiashara na mmiliki wa viwanda vya nguo nchini, Adam Zuku amesema licha ya tume hiyo kusheheni wajumbe wenye uzoefu mkubwa katika kodi, lakini hakuna uwakilishi wa upande wa walalamikaji. 

“Ni jambo zuri ambalo Rais amelifanya, ameunda tume ya watu wa juu wenye utaalamu wa kodi na ukaguzi wa hesabu.

“Hata hivyo, nina wasiwasi kwamba hawa watu wote ni bureaucratic (maofisa), nina wasiwasi kwamba hakuna hata mmoja aliyewahi kufanya biashara,” amesema.

Amesema kutokana malalalamiko yaliyoibuliwa kwenye Baraza la Biashara ambalo mwenyekiti wake ni Rais Samia, alipaswa kuangalia uwakilishi.

“Naona washauri wake hawakumwelekeza kutatua tatizo vizuri. Ni kweli hawa watu ni wazuri, lakini naona matakwa ya Rais hayatafikiwa hasa katika usimamizi wa kodi na kuongeza wigo wa walipa kodi,” amesema.

Ameshauri ili kuongeza ushirikishwaji wa walengwa, pamoja na tume hiyo, ziundwe kamati ndogo kutoka kwenye makundi, ili nayo yashiriki.

“Hiyo tume ina upungufu kwa sababu walengwa hawamo, wakiwamo vijana, wazalishaji viwandani kupitia (Shirikisho la wenye Viwanda – CTI), wafanyabiashara wa kawaida kote nchini kupitia taasisi zinazowawakilisha kama (Chemba ya Wafanyabiashara na Kilimo (TCCIA),” amesema na kuongeza;

 “Vijana wanamaliza vyuo vikuu hawana kazi, kidato cha sita hawana kazi, kidato cha nne hawana kazi na darasa la saba hawana kazi.

“Tukipata kuwa na wigo mkubwa wa kodi, tuwalenge hawa, tuwafanye wafanye shughuli zozote za kuzlisha mali, ili tukusanye kodi.

“Kinachotakiwa ni kuwalea ili wakifika kwenye kiwango fulani ndipo unaweza kuwalipisha kodi,” anasema. 

Amesema hata kama tume hiyo itakwenda kuzungumza na makundi yote, lakini kuna tofauti ya kuongea nao na kuwakilishwa moja kwa moja.

“Ni muhimu kuwakilishwa kwenye tume ambayo mwisho wake itatoa uamuzi, ili kulinda yale wanayotaka yawemo.

“Kodi ni suala la Serikali dhidi ya walipa kodi, sasa hawa ni watumishi waandamizi wa Serikali, unategemea wana mtazamo gani chanya kwa walipa kodi?

“Rais anatarajia kupata mawazo yanayolingana, hapo utapata mawazo yanayolingana?” amehoji.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa wafanyabiashara wa Kariakoo, Martin Mbwana licha ya kuwa na matumaini na tume hiyo, amesema inapaswa kwenda kugusa watu wa chini kwenye kero yenyewe.

“Tunaomba wateremke huku chini wakutane na uhalisia, wakutane na wafanyabiashara moja kwa moja,” amesema.

Ametaja moja ya kero katika biashara yao akisema ni mfumo wa utendaji katika ukusanyaji wa kodi, akishauri kufanyika mabadiliko katika mtalaa wa masomo ya kodi vyuoni.

“Inawezekana huku tukabadilisha sheria, lakini kule vyuoni wanapikwa kwa sheria za kikoloni. Kwa mfano Jeshi la Polisi wamebadilika kutoka Jeshi la Polisi wamekwenda kwenye Polisi Jamii, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) nao wabadilike.

“Benki wametoka kujifungia wenyewe ndani, sasa wametoka nje, leo unamkuta wakala wa benki anafanya kazi asilimia 75 ya benki, maana yake wameshirikishana.

“Mfumo wa sheria uiwezeshe TRA nayo ishirikishe jamii. Sisi tulioko huku chini tunaweza kushauri namna ya kuongeza wigo wa walipa kodi,” amesema.

Naye Meneja Programu wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Kennedy Rwehumbiza amesema malalamiko ya sekta binafsi ni sera za kodi na utaratibu wa ukusanyaji.

“Hiyo tume jukumu lake liwe kutibu malalamiko ya sekta binafsi, inawezekana ni TRA au wizara vinakuwa vikwazo, basi hayo yote yapatiwe ufumbuzi,” ameshauri.

Related Posts